Wakala ya Serikali Mtandao imepata ushindi wa nafasi ya nne na kutunukiwa Tuzo ya Taasisi Zinazosimamiwa Vizuri Kiutendaji (Best Managed MDA) kati ya taasisi zaidi ya 70 za Serikali zilizokuwa kwenye kinyanganyiro hicho.
Tuzo hiyo ilikabidhiwa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Mhe. Ali Hassan Mwinyi kwa Mtendaji Mkuu wa Wakala Dkt. Jabiri Bakari wakati wa kilele cha Wiki ya Utumishi wa Umma Juni 23, 2015 kwenye viwanja vya Mnazi mmoja jijini Dar es salaam.
“Kwa mwaka huu tumepata nafasi ya nne, ninaamini kuwa kwa mwaka 2016 tutafanya vizuri zaidi kwa kuwa tutafanya maandalizi mapema” alisema Dkt. Bakari.
Hata hivyo Dkt. Bakari aliwapongeza watumishi wa Wakala kwa kufanya jitihada mbalimbali ambazo zimefanikisha kupata ushindi huo.
Naye Meneja wa kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano Bi. Suzan Mshakangoto alisema Wakala imepiga hatua kubwa ukilinganisha na mwaka jana.
“Mwaka huu tumekuwa nafasi ya nne tumepiga hatua kubwa kwani mwaka jana tulikuwa nafasi ya tisa, na tunaanza kujipanga mapema zaidi ili mwaka 2016 tushike nafasi ya kwanza” alisema Suzan.
Maonyesho hayo yenye kauli mbiu “Utumishi wa Umma katika Bara la Afrika ni Chachu ya Kuwawezesha Wanawake, Kuongeza Ubunifu na Kuboresha Utoaji Huduma kwa Umma” yalianza Juni 16 nakumalizika Juni 23, 2015.