Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, kupitia Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), imetengeneza Mfumo wa kidigitali ujulikanao kama e-Mrejesho, unaomuwezesha mwananchi kuwasilisha malalamiko, kero, maoni, mapendekezo, au maulizo moja kwa moja kwenye Taasisi /Wizara husika sambamba na kufuatilia utekelezaji wake.
Mfumo huo wa kidigitali una lengo la kumsaidia mwananchi kupunguza gharama pamoja na kuokoa muda wa kutembea umbali mrefu ili kuwasilisha maoni, mapendekezo au kufuatilia malalamiko yake.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama (Mb) amesema kuwa, Mfumo wa e-Mrejesho ni suluhisho kwa wananchi kwani unamuwezesha mwananchi kuwasiliana na Serikali moja kwa moja na kuwasilisha maoni yake kupitia simu ya kiganjani.
Aidha, Waziri Mhagama ameeleza kuwa, Mfumo wa e-Mrejesho umeongeza ufanisi wa utendaji kazi Serikalini katika utoaji wa huduma kwa wakati na kwa ubora, kwani watumishi wa umma wanaweza kujibu malalamiko au maoni ya wananchi wengi kwa muda mfupi kupitia mfumo huo.
Waziri Mhagama amesisitiza kuwa, kutokana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia Mfumo wa e-Mrejesho umekuwa ni fursa nzuri kwa wananchi kuwasiliana na Serikali kwa urahisi na haraka zaidi hivyo amewataka wananchi kutoogopa kuutumia mfumo huo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao, Eng. Benedict Ndomba amesema kuwa, Mfumo wa e-Mrejesho ni salama na umezingatia usiri mkubwa wa taarifa kwani mwananchi anapowasilisha maoni au malalamiko yake, mfumo unampa nafasi ya kuchagua kujulikana au kutojulikana kwa kuandika au kutoandika taarifa zake binafsi.
“Napenda kuwahakikisha kuwa, mfumo huu ni salama kutumia kwani unampa nafasi mwananchi ya kuchagua kujulikana kwa kuandika majina yake na namba za simu na kama hatopenda basi ataacha wazi”, amesisitiza Eng. Ndomba.
Aidha, Mkurugenzi amesema kuwa, Mfumo huu wa e-Mrejesho unaziunganisha Taasisi zote za Serikali hivyo, Taasisi kwa Taasisi zinaweza kubadilishana taarifa za malalamiko au maoni yanayotolewa na wananchi na pia Serikali inaweza kupata takwimu za malalamiko hayo.
Eng. Ndomba ametoa wito kwa wananchi wote kuupenda na kuutumia mfumo huo wa kidijitali ili kuongeza ufanisi katika Taasisi za Umma kwenye utoaji wa huduma kwa jamii sambamba na kuunga mkono Jitihada za Serikali Mtandao.
Mfumo wa e-mrejesho unapatikana katika tovuti ya www.emrejesho.go.tz, au kwa kupakua ‘application’ ya eMrejesho kwa kutumia simu janja au kupiga namba ya msimbo *152*00# kisha chagua namba 9, kisha chagua 2 na kisha fuata maelekezo