Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Mha. Benedict Ndomba, amesema kuwa, jumla ya taasisi za umma 109 zimeunganishwa katika Mfumo Mkuu wa Ubadilishanaji taarifa Serikalini ujulikanao kama Government Enterprises Service Bus (GovESB), na tayari mifumo ya TEHAMA 117 imesajiliwa katika mfumo huo.
Mfumo wa GovESB, ni mfumo wa kielektroniki unaounganisha mifumo ya TEHAMA ya taasisi za umma iweze kusomana na kubadilishana taarifa kwa usalama, ili kupunguza urudufu wa mifumo, kuongeza ufanisi wa utendaji kazi na kupunguza gharama za uendeshaji.
Akizungumza katika mkutano na Waandishi wa Habari leo jijini Dodoma, Ndomba amesema kuwa, miongoni mwa taasisi zilizojiunga na mfumo huo ni Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Wakala wa Leseni za Biashara (BRELLA) na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA).
“Mfumo wa GovESB, umetengenezwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kwa kuzingatia kifungu cha 48 (2) cha Sheria ya Serikali Mtandao Na. 10 ya Mwaka 2019, kinachoitaka Mamlaka ya Serikali Mtandao, kuanzisha na kuendesha Mfumo unaowezesha mifumo ya TEHAMA Serikalini kuwasiliana na kubadilishana taarifa”, amefafanua Ndomba.
Ameongeza kuwa, sambamba na utekelezaji wa takwa la kisheria pia, ujenzi wa mfumo huo ni utekelezaji wa agizo la Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, la kuhakikisha mifumo ya TEHAMA katika taasisi za umma inaunganishwa na kubadilishana taarifa.
“Mfumo huu umeleta mafanikio katika sekta mbalimbali ikiwemo ya sheria, ambapo taasisi za hakinijnai yaani Mahakama, Jeshi la Polisi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Ofisi ya Taifa ya Mashitaka (NPS), zimejiunga na zinabadilishana taarifa kupitia GoVESB na hivyo kusaidia kuongeza ufanisi wa utendaji kazi, uwazi pamoja na utoaji haki kwa wananchi kwa wakati”, amesisitiza Ndomba.
Sanjari na hilo, Ndomba amebainisha kuwa e-GA, kwa kushirikiana na taasisi nyingine za umma ikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Wizara ya Fedha, imesanifu na kujenga Mfumo wa Pamoja wa Kielekroniki wa Uondoshaji wa Shehena Maeneo ya Forodha (Tanzania Electronic Single Window System - TeSWS).
Amesema kwamba, Mfumo wa TeSWS ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara nchini – MKUMBI (Blueprint), ili kuwezesha wafanyabiashara kukamilisha maombi ya vibali na maandalizi ya malipo ya kodi za forodha kidijitali, bila kulazimika kufika kwenye ofisi zinazohusika.
“Mfumo wa TeSWS unaruhusu wadau wa biashara na wasafirishaji kuwasilisha mara moja tu kwenye mfumo taarifa za kiforodha na shehena zinazoingia na kutoka nchini, pamoja na zile zinazopita nchini kwenda nchi jirani ambapo kila mdau anayehusika ataziona na kuzifanyia kazi kwenye mfumo” ameeleza Ndomba.
Amebainisha kuwa, mfumo wa TeSWS una awamu tatu ambapo awamu ya kwanza inahusu moduli za taratibu za forodha ‘Customs Procedures’ na zile za taasisi za Udhibiti na Ukaguzi, na Malipo ya Huduma na tayari inatumika kwa Bandari ya Dar Es Salaam na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, ambapo kampuni za wakala wa forodha (CFA) 1,496 sawa na asilimia 100 pamoja na makampuni ya watunza shehena 246 zinatumia mfumo huu.
Awamu ya pili imeanza kutumika na inahusu moduli za taratibu za ujio wa meli na uondoshaji wa shehena maeneo ya forodha ‘Cargo Management’, na awamu ya tatu inahusu moduli za taratibu nyingine ndogondogo za forodha ndani ya TRA, TPA, Posta na Viwanja vya Ndege na sasa ipo katika hatua ya majaribio.
Kwa upande wa ubadilishanaji wa taarifa kati ya mifumo ya TEHAMA ya Serikali na ya Sekta binafsi, Ndomba amesema kuwa, ubadilishanaji wa taarifa kati ya sekta hizo, unawezeshwa kadiri ya mahitaji yanavyojitokeza.
“Mfumo wa malipo ya Serikali (GePG) umeunganishwa na Benki zote nchini pamoja na Kampuni zote za Simu za Mikononi, ili kuwezesha huduma ya malipo ya Serikali kupitia simu za mikononi pia, Mfumo wa Huduma za Serikali kupitia Simu za Mkononi (Government Mobile Platform -mGov) umeunganishwa na mifumo ya kampuni zote za simu nchini, na kuwezesha kutoa huduma za Serikali, kwa njia ya simu za mkononi”, amesema Ndomba na kuongeza kuwa,
“Ili kuhakikisha taasisi nyingi zaidi zinajiunga na mfumo wa GovESB na kubadilishana taarifa kupitia mfumo huo, tunaendelea kufanya jitihada mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufanya vikao na taasisi za umma ambapo kati ya Agosti na Novemba 2023, tumefanya vikao na taasisi 55 na sisi tupo tayari muda wowote kuziwezesha taasisi za umma zinazohitaji kujiunga na GoVESB ili ziweze kubadilishana taarifa”, amesema Ndomba.