emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

e-GA yaweka Mikakati Madhubuti ya Kuijenga Serikali Kidijitali


e-GA yaweka Mikakati Madhubuti ya Kuijenga Serikali Kidijitali


Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) itaendele imeweka mikakati madhubuti ya utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao itakayosaidia kuimarisha na kuijenga serikali kidijitali.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), Mhandisi Benedict Ndomba wakati alipofanya mkutano na waandishi wa habari, kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka.

“Katika kipindi cha miaka 10 ijayo, e-GA itaandaa na kutekeleza mikakati itakayojiwekea ili kuimarisha zaidi utekelezaji wa jitihada za Serikali kimtandao na kuhahikisha kuwa Taasisi za Umma zinatoa huduma kwa wananchi kwa njia ya kidijitali”, alisema Ndomba..

Aidha, Ndomba alifafanua kuwa, utekelezaji wa mikakati hiyo utasaidia uwepo wa sehemu moja ambayo huduma zote za mtandao zitakuwa zinapatikana, pamoja na kuwa na uwezo wa kutumia teknolojia mpya zinazoibuka, hasa zile za akili bandia, sarafu za kidijiti na teknolojia za kifedha, ili kuwezesha maboresho ya kiutendaji katika Taasisi za Umma na utoaji wa huduma kwa Umma.

Ndomba aliongeza kuwa, kupitia utekelezaji wa mikakati hiyo Mamlaka itahakikisha kuwa, idadi ya vijana wa kitanzania wenye uwezo mkubwa wa ubunifu katika utekelezaji wa jitihada za Serikali mtandao inaongezeka pamoja na uwepo wa Mifumo na Miundombinu ya Serikali mtandao iliyo bora na imara zaidi.

“Ili kufikia yote haya katika kipindi kijacho, Mamlaka itaendela kuunganisha Mifumo ya Taasisi za Umma kwenye Mfumo wa Serikali wa kubadilishana Taarifa (Government Enterprise Service Bus - GovESB) na kuendeleza shughuli za tafiti na ubunifu katika matumizi ya teknolojia mpya za TEHAMA ili kuibua huduma mpya kwa umma na kuwezesha matumizi sahihi ya teknolojia”, alisema Ndomba.

Katika kuimarisha Serikali Mtandao nchini, Mamlaka itaendelea kupitia na kutathmini hali ya usalama wa Mifumo na Miundombinu ya Serikali Mtandao na kuzishauri Taasisi za Umma katika maeneo ya kuboresha, pamoja na kufuatilia utekelezaji wake ili kuhakikisha kuwa Mifumo na Miundombinu ya TEHAMA inafanya kazi wakati wote kwa ufanisi na usalama”, alisisitiza Ndomba.

Aidha, Ndomba alisema kuwa, Mamlaka imejipanga na itaendelea kutekeleza majukumu yake ipasavyo kwa kusimamia uzingatiaji wa Sera, Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao kwa Taasisi za Umma ili kujenga Serikali ya Kidijitali.