emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

e-GA YATOA ELIMU YA SERIKALI MTANDAO KWA VIZIWI


e-GA YATOA ELIMU YA SERIKALI MTANDAO KWA VIZIWI


Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), imetoa elimu ya matumizi ya Serikali Mtandao kwa viziwi wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Kimataifa ya Viziwi 2024, ambayo kitaifa yalifanyika mkoani Shinyanga Septemba hadi mwaka huu.

Katika kongamano hilo, e-GA ilitoa elimu kuhusu Serikali Mtandao na namna inavyoweza kurahisisha upatikanaji wa huduma za Serikali kupitia mifumo mbalimbali ya TEHAMA kwa watu wenye mahitaji maalumu wakiwemo Viziwi.

Moja ya mfumo uliowasilishwa ni Mfumo wa Huduma za Serikali kupitia Simu ya Mkononi (mGov), ambapo mwananchi anaweza kupata huduma mbalimbali za Serikali kupitia simu ya mkononi kwa kupiga namba ya msimbo *152*00#.

Akizungumza katika kongamano hilo Afisa TEHAMA kutoka Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Bw.Patrick Mdagano, amebainisha kuwa Mamlaka ya Serikali Mtandao inaendelea kubuni mifumo ambayo itarahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi wa makundi yote katika jamii.

“Kwa kutumia mfumo wa mGov ambao unapatikana hata kwenye simu ya kawaida ‘kiswaswadu’ kupitia namba ya msimbo *152*00# unaweza kupata huduma za serikali ukiwa mahali popote”, alifafanua Bw. Mdagano.

Vilevile, Bw.Mdagano alieleza kuhusu mfumo wa e-Mrejesho unaotumika kama kiungo cha mawasiliano kati ya wananchi na Serikali, na kuwataka Viziwi kutumia mfumo huo kuwasilisha changamoto zinazowakabili katika upatikanaji wa huduma mbalimbali za Serikali, ili ziweze kupatiwa suluhisho kwa haraka katika taasisi husika.

Mfumo wa e-Mrejesho unapatikana kwa njia tatu ambazo ni kupitia simu ya mkononi kwa kubofya *152*00# na kisha kuchagua namba 8 na kisha namba 2, njia zingine ni kupitia simu janja kwa kupakua Aplikesheni (Mobile App) ya e-Mrejesho inayopatikana kwenye Play Store na Apple Apps Store, na kwa njia ya Tovuti ya emrejesho.gov.go.tz.

Naye Afisa Sheria wa e-GA Bw.Watson Kimbe alisema kuwa, Sheria ya Serikali Mtandao Na. 10 ya mwaka 2019, inatambua uwepo wa watu wenye mahitaji maalumu wakiwemo Viziwi katika utoaji wa huduma bora za Serikali Mtandao nchini.

Aliongeza kuwa, kifungu cha 28 (e) cha sheria hiyo kinatoa malekezo kwa taasisi za umma kuweka mazingira rafiki ya utoaji wa huduma za serikali mtandao kwa watu wenye mahitaji maalumu.

Kwa upande wake Mjumbe wa Bodi ya Utendaji kutoka Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA), Subira Upurute ameipongeza Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kwa jitihada zake za kuyafikia makundi yenye mahitaji maalumu.

“Kwa miaka mingi iliyopita kundi la Viziwi limekuwa ni kundi la mwisho katika kupata taarifa mbalimbali, lakini tunaishukuru e-GA kwa kuwa karibu na kundi hili na kutujengea uelewa kuhusu dhana ya Serikali Mtandao”, alisema Bi.Upurute.

Alibainisha kuwa, Serikali Mtandao imewasaidia Viziwi katika upatikanaji wa huduma mbalimbali za serikali ikiwemo ulipaji wa Ankara za umeme na maji kupitia simu ya mkononi.

Aidha,Bi Upurute ameishukuru e-GA kwa kushiriki katika maadhimisho hayo ikiwa ni dhamira ya wazi ya Mamlaka ya Serikali Mtandao, kuunga mkono jitahada za CHAVITA katika kujenga ustawi wa Viziwi katika ulimwengu wa kidijiti.