Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mh. Jenista Mhagama, ameitaka Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kuwa kioo na kitovu cha mifumo ya TEHAMA nchini.
Mh. Jenista ametoa kauli hiyo leo katika ofisi za Bunge jijini Dodoma, mara baada ya Mkurugenzi Mkuu wa e-GA Mhandisi Benedict Ndomba kuwasilisha mada kuhusu Usalama wa Serikali Mtandao kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, iliyolenga kuwajengea uwezo viongozi hao kuhusu usalama wa mitandao.
“Tunataka e-GA iongeze ubunifu na ujengaji wa mifumo ya TEHAMA ili kuwa kitovu cha utafiti kwa ukanda wa Afrika Mashariki, pamoja na kazi kubwa na nzuri ambayo e-GA inaifanya lakini inapaswa kuongeza juhudi zaidi”, alisema Mh. Jenista.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Mh. Daniel Sillo (Mb) ameeleza kuridhishwa na utendaji kazi wa e-GA na kuitaka kuendelea kuwa wabunifu na kuhakikisha usalama wa mifumo ya TEHAMA unakuwepo ili kudhibiti upotevu wa fedha za Serikali hasa katika Halmashauri
Akiwasilisha mada kuhusu Usalama wa Serikali Mtandao, Mhandisi Ndomba ameeleza kuwa, hivi sasa kuna ongezeko la vitendo vya udukuzi wa taarifa mbalimbali ambapo, amewasihi wabunge na wananchi kwa jumla kuwa makini na matumizi ya TEHAMA pamoja na taarifa wanazopata mitandaoni.
Aidha, Wajumbe wa Kamati hiyo wameipongeza e-GA kwa kutekeleza vema majukumu yake na kuitaka kutoa elimu kuhusu usalama wa mitandao kwa wananchi ili kuwajengea uelewa na kuweza kulinda taarifa zao katika mitandao.