emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

e-GA YAPATA ITHIBATI YA UBORA KIMATAIFA (ISO 9001:2015)


e-GA YAPATA ITHIBATI YA UBORA KIMATAIFA (ISO 9001:2015)


Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), imethibitishwa kuwa Taasisi inayofuata viwango vya Kimataifa (ISO) katika kuratibu, kusimamia na kukuza jitihada za Serikali Mtandao, pamoja na kuhimiza utekelezaji wa Sera, Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao kwa Taasisi za Umma kulingana na Kiwango cha Ubora wa Kimataifa (ISO 9001:2015).

Hayo yameshwabaini na Kaimu Meneja wa Kitengo cha Usimamizi wa Vihatarishi na Ubora wa TEHAMA wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Bi. Farida Juma, alipofanya mahojiano maalum na mwandishi wetu Machi 20 mwaka huu ofisini kwake jijini Dodoma.

“Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), tumepokea cheti cha uthibitisho wa kiwango cha ubora wa kimataifa na sasa tunatambulika kimataifa kama Taasisi inayofuata viwango vya ubora wa kimataifa katika kuratibu na kusimamia utoaji wa huduma na mifumo salama ya kieletroni kwa Taasisi za Umma”, alisema Farida.

Aliongeza kuwa, katika ripoti ya mwaka 2022 ya utafiti uliofanywa na Benki ya Dunia (WB) kuhusu Ukomavu wa Matumizi ya Teknolojia Duniani katika utoaji wa huduma za Serikali na ushirikishwaji wa wananchi (GovTech Maturity Index), Tanzania ilitajwa kushika nafasi ya pili barani Afrika na nafasi ya kwanza Afrika Mashariki, na hivyo uthibitisho huo wa ISO 9001:2015 ni moja ya hatua kubwa ambazo Mamlaka imepiga katika mafanikio yake.

Alisema kuwa, kupata uthibitisho huo wa ISO 9001:2015 kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS), ni hatua muhimu katika kuonyesha msimamo wa Mamlaka wa kutoa huduma bora zaidi za TEHAMA kwa Taasisi za Umma na kuboresha utendaji kazi.

“Lengo letu ni kuendelea kuimarisha utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao kwa Taasisi za Umma ili kuboresha utendaji kazi Serikalini na utoaji wa huduma za Serikali kidijitali na hivyo kupunguza muda wa kutoa huduma na kuongeza ufanisi”, alisisita Bi. Farida.

Aidha, alibainisha kuwa mchakato wa kupata cheti hicho ulianza kwa watumishi wa e-GA kupatiwa mafunzo na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), ili kuwawezesha watumishi hao kukidhi vigezo vya utoaji huduma kwa wateja wake kulingana na matakwa ya kiwango cha ubora.

Aliongeza kuwa, e-GA imejizatiti kutoa mifumo bora na salama ya kieletroniki kwa Taasisi za Umma na kuendelea kuboresha huduma zake ili kukidhi mahitaji ya kisheria, viwango vya kimataifa na matarajio ya wateja wake.

“Tutahakikisha ufanisi unaongezeka katika kutoa huduma thabiti na kukidhi mahitaji na matarajio ya wateja na wadau wetu kulingana na viwango vya ubora wa kimataifa”alisisitiza Bi. Farida

Alisisitiza kuwa, Mamlaka itaendelea kutoa rasilimali zinazohitajika kwa ajili ya utekelezaji wa mfumo wa usimamizi wa ubora ulioanzishwa kulingana na mahitaji ya viwango vyaUbora wa Kimataifa (ISO ).

Kiwango cha ISO 900:2015 ni mfumo wa usimamizi uliotengenezwa na Shirika la Viwango vya Kimataifa (ISO) linalolenga seti ya mahitaji ambayo Taasisi au Shirika linapaswa kufikia katika mfumo wa ubora ili kupata hati ya ISO 9001:2015.