Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) imetoa mchango wa kompyuta 10 kwa Jeshi la Polisi nchini, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha matumizi ya teknolojia katika utoaji wa haki kwa wananchi.
Makabidhiano hayo yalifanyika jana katika Ofisi za Mamlaka jijini Dar es Salaam ambapo kwa upande wa e-GA Bw. Benjamin Dotto Mkurugenzi wa Miundombinu na Uwezeshaji wa TEHAMA alikabidhi komputa hizo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu Mhandisi. Benedict Ndomba.
Akiongea wakati wa makabidhiano hayo, Bw. Dotto alisema kuwa, e-GA imekuwa ikishirikiana na Taasisi mbalimbali za Umma likiwemo Jeshi la Polisi, katika kuhakikisha matumizi ya Teknolojia yanarahisisha utendaji kazi wa Taasisi na utoaji wa huduma kwa umma.
“Teknolojia hurahisisha mchakato wa utoaji wa haki na sisi e-GA tukaona ni vizuri kuchangia kwa kutoa kompyuta hizi ili zirahisishe mchakato wa haki jinai katika Jeshi la Polisi”, alisema Dotto.
Kwa upande wake, Mkuu wa TEHAMA wa Jeshi la Polisi Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Justus Mafuru alisema kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliagiza kutengeneza Mfumo wa haki jinai ambao tayari umekwishatengenezwa.
“Kwa niaba ya IGP tunaishukuru e-GA kwa mchango huu wa kompyuta ambao utasaidia upatikanaji wa haki kwa wananchi kwa urahisi na haraka kupitia Teknolojia na kwakuwa Mfumo wa hakijinai umekwishatengenezwa kwa sasa tunahitaji vifaa”, alisema ACP Mafuru.
Mamlaka ya Serikali Mtandao ni Taasisi ya Umma iliyoanzishwa kwa Sheria ya Serikali Mtandao Na. 10 ya mwaka 2019, ikiwa na majukumu ya kuratibu, kusimamia na kukuza jitihada za Serikali Mtandao, pamoja na kusimamia uzingatiaji wa Sera, Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao katika taasisi za umma.