“Uadilifu na ubunifu kwa utoaji wa huduma bora kwa umma” huu ndio moto wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), unaoangaza njia inayochochea bunifu mbalimbali za TEHAMA zitakazosaidia kuboresha utoaji wa huduma za Serikali kidijitali.
Ili kufikia mafanikio haya, Oktoba 2019 e-GA ilianzisha Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao (eGOVRIDC), kwa lengo la kuimarisha na kukuza tafiti pamoja na bunifu za TEHAMA, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta hiyo.
Miongoni mwa wadau hao ni Taasisi za Vyuo Vikuu ambapo, hadi sasa e-GA imeingia Mkataba wa Makubaliano (MOU) na Taasisi 14 za Vyuo vikuu nchini zinazotoa mafunzo ya TEHAMA kwa ngazi mbalimbali.
Taasisi hizo ni pamoja na Chuo Kikuu Dodoma (UDOM), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu Mzumbe, Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Chuo cha Teknolojia cha Dar es Salaam (DIT), Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) n.k.
Aidha, malengo ya makubaliano hayo ni pamoja na kuratibu shughuli za utafiti wa Serikali Mtandao kwa kuweka mazingira wezeshi ya tafiti hizo, kuhimiza ubunifu kwa vijana wazawa katika eneo la TEHAMA, kupunguza utegemezi wa wakandarasi wa nje na kutengeneza mifumo ya TEHAMA iliyo salama zaidi (salama dhidi ya matishio ya kimtandao).
Kupitia kituo hiki, vijana mbalimbali wa kitanzania wanaosoma fani ya TEHAMA katika Vyuo hivyo, wamepata fursa ya kujifunza kwa vitendo, na hatimaye kuibua na kukuza vipaji vyao katika eneo la uvumbuzi wa mifumo mbalimbali ya TEHAMA, itakayosaidia kutatua changamoto za utendaji kazi Serikalini na kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Meneja wa Huduma za Sheria Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Rafael Rutahiwa anasema kuwa, makubaliano ya ushirikiano kati ya e-GA na Vyuo Vikuu yamesaidia kuziba pengo kati ya wahitimu wa Vyuo Vikuu na ujuzi unaohitajika katika soko la ajira.
Anabainisha kuwa, ushirikiano huo umesaidia Vyuo Vikuu nchini kubaini maeneo yanayotakiwa kuboreshwa katika mitaala ya kufundishia ili kutengeneza vijana wanaoendana na soko la ajira.
“Vilevile, ushirikiano wetu na Vyuo Vikuu umesaidia kutoa nafasi kwa vijana wa Vyuo hivyo kujifunza kwa vitendo na kuweza kushindana katika soko la ajira ndani na nje ya nchi, pamoja na kuwawezesha kujiajiri wenyewe kwakuwa tayari wanakuwa na ujuzi unaohitajika sokoni”, anasisitiza SACP Rutahiwa.
Sambamba na hilo, SACP Rutahiwa anabainisha kuwa mafunzo yanayotolewa kwa vijana hao yamekuwa yakihusisha matumizi ya teknolojia huria ‘open source’ katika utengenezaji wa mifumo rahisi ambayo inaweza kutumiwa na Serikali na hivyo kuondoa urudufu wa mifumo.
“Pamoja na utoaji wa fursa ya mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wa Vyuo Vikuu, pia tunashirikiana na vyuo hivyo katika tafiti mbalimbali kwenye eneo la TEHAMA ambazo zinalenga kuimarisha Serikali Mtandao”, anasema Rutaihiwa.
Aidha, Rutahiwa anabainisha kwamba kupitia eGOVRIDC, Serikali imeweza kuondokana na utegemezi wa utengenezaji wa mifumo ya TEHAMA kwa kutumia wakandarasi wa kigeni ambao hapo awali walitengeneza mifumo hiyo kwa gharama kubwa, huku baadhi yao wakishindwa kutengeneza mifumo kulingana na taratibu za kiutendaji ndani ya taasisi, na hivyo mifumo hiyo kushindwa kutatua matatizo ya taasisi husika na kusababisha urudufu wa mifumo.
“Kituo chetu cha utafiti na ubunifu kinabuni na kutengeneza mifumo mbalimbali ya TEHAMA inayoweza kutumika Serikalini na kutatua changamoto zilizopo, tunahakikisha kabla ya utengenezaji tunafahamu taratibu za utendaji wa taasisi husika na mwisho kabisa ni lazima mifumo hiyo itatue changamoto zilizokuwepo”, anasisitiza Rutahiwa.
Ametaja baadhi ya mifumo iliyobuniwa na kutengenezwa na kituo hicho, ambayo inatumiwa na taasisi mbalimbali za umma ni pamoja na mfumo wa uendeshaji vikao wa e-Mikutano, Mfumo wa uandaandaaji na uendeshaji wa vikao vya Menejimenti na Halmashauri wa e-Board pamoja na mfumo wa kutuma na kupokea maoni au pongezi Serikalini wa e-Mrejesho.
“Ushirikiano wetu sisi e-GA na Vyuo Vikuu umeleta matokeo chanya na mazuri, na sisi e-GA tutandelea kuimarisha ushirikiano huu ili kukuza ujuzi na vipaji kwa vijana wa Kitanzania wabunifu katika TEHAMA na hatimaye tuweze kujenga kizazi chenye umahiri katika dijitali”, anasema Rutahiwa.
Kwa upande wake Meneja wa Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao (eGovRIDC) Dkt. Jaha Mvulla, anasema lengo kubwa la kituo hiki ni kufanya utafiti na ubunifu kwenye eneo la TEHAMA, kuibua teknolojia zitakazosaidia Serikali katika utendaji kazi lakini pia kukuza na kuendeleza vijana wabunifu kutoka vyuoni.
Anabainisha kuwa, e-GA inawapa fursa wanafunzi wa kada ya TEHAMA kupata picha halisi ya masomo wanayoyasoma pamoja na hali halisi ya sekta husika ilivyo katika soko shindani la ajira, kwa kuwajengea uwezo wanafunzi na kuchochea ubunifu na vipaji vyao.
“Programu mbalimbali zinazoendeshwa na kituo hiki zimewasaidia wanafunzi wengi wa vyuo vikuu, kuongeza ujuzi na uzoefu katika kuzielewa teknolojia mpya ili kuchochea maendeleo na mageuzi makubwa ya Serikali ya kidigitali, kutatua changamoto za kiteknolojia na kubuni mifumo ya TEHAMA inayoweza kutumika Serikalini kwa lengo la kuongeza ufanisi wa utendaji kazi”, anasisitiza Dkt. Jaha na kuongeza kuwa,
“e-GA inajivunia uvumbuzi wa mfumo tumizi wa e-Mrejesho ambao tayari umetambuliwa na Benki ya Dunia (WB) pamoja na Umoja wa Mataifa (UN) kama mfumo bora unaotoa ushirikishaji kwa wananchi kwakuwa wananchi wanaweza kutuma maoni, malalamiko au pongezi kwenda kwenye taasisi za umma pamoja na kufuatilia utekelezaji wake”, anasisitiza Dkt.Jaha.
Mfumo mwingine unaotokana na zao la kituo chetu cha eGOVRIDC ni mfumo wa kuwezesha uratibu wa shughuli za uandaaji wa vikao mbalimbali vya bodi na menejimenti, ujulikanao kama e-Board, ambao hadi sasa taasisi zaidi ya 60 zinatumia mfumo huu, zikiwemo Wizara, Taasisi na halmashauri mbalimbali.
“Tunajivunia kuona vijana wengi waliopata mafunzo kutoka hapa eGOVRIDC, wamekuwa mahiri katika maeneo mbalimbali ya teknolojia na kupata fursa za ajira ndani na nje ya nchi, hii inadhihirisha kuwa, Mamlaka imewasaidia na kuwajengea uwezo mkubwa vijana hawa wa kuweza kushindana katika soko la ajira duniani”, anasema Dkt. Jaha.
Pamoja na mafanikio hayo yaliyopatikana kupitia kituo hiki, e-GA imeandaa mpango endelevu wa kutatua changamoto zilizopo kupitia tafiti na bunifu mbalimbali kwenye matumizi ya teknolojia mpya zinazochipukia ‘Emerging Technologies’ na kujivunia baadhi ya mifumo iliyotengenezwa kupitia teknolojia hizo ikiwemo Internet of Things (IOT), Blockchain, Machine Learning na Artificial Intelligence (AI).
“e-GA itaendelea kuboresha miundombinu ya kituo na mazingira yake ikiwemo kuongeza vifaa tumizi kwa ajili ya kuwezesha mafunzo kwa vitendo kufanyika kwa ukamilifu, ili kukiwezesha kituo hiki kiendelee kufanya kazi zake za utafiti na ubunifu kwa ufanisi zaidi”, anasema Dkt. Jaha.
Mmoja wa washiriki wa programu maalumu ya mafunzo kazini ‘Internship’ inayoendeshwa na kituo hiki Bw. Claud Charles, ameishukuru e-GA kwa kutoa fursa ya mafunzo hayo yaliyomsaidia kutengeneza moja ya mfumo utakaoisaidia Serikali katika utendaji kazi wake.
“Naishukuru sana e-GA kwa kunipa nafasi hii kwani kwa kushirikiana na watumishi wake tuliweza kutengeneza mfumo wa Webguard utakaosaidia kufuatilia ufanisi wa mifumo mingine ya Serikali ikiwemo tovuti za Serikali na kubaini kiwa zipo sawa au la”, anasema Bw. Claud.
Aidha, Bw. Claud ameiomba e-GA kuendeleza ushirikiano uliopo na Vyuo Vikuu nchini katika shughuli mbalimbali za utafiti na ubunifu ili kuibua vijana wenye vipaji katika TEHAMA.
Naye Bi. Miriam shaka, ambaye pia ni mshiriki wa program hiyo anabainisha kwamba anatarajia kuona mafunzo wanayoendelea kuyapata yanawasaidia kuzielewa teknolojia mpya, na kutumia teknolojia hizo katika uvumbuzi wa mifumo mbalimbali itakayosaidia Serikali katika utendaji wa kazi.
“Nafasi hii tuliyopata ni muhimu sana kwetu lakini pia kwa manufaa ya taifa letu, hivyo tutaitumia kujifunza na kupata ujuzi utakaosaidia kuleta maendeleo kwa taifa letu sambamba na kukuza uchumi wetu”, anasisitiza Miriam.
Hadi sasa takribani vijana 300 wamepata fursa na kunufaika na programu inayoendeshwa katika kituo hiki, huku matarajio ya e-GA yakiwa ni kujenga kituo kikubwa cha utafiti na ubunifu kitakachoweza kuchukua wanafunzi wengi zaidi wa mafunzo kwa vitendo kwa mara moja.
MWISHO