emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

e-GA KUIMARISHA MAHUSIANO NA CHUO KIKUU CHA MZUMBE


e-GA KUIMARISHA MAHUSIANO NA CHUO KIKUU CHA MZUMBE


Mamlaka ya Serikali Mtanda (e-GA) inalenga kuimarisha zaidi uhusiano wake na Chuo Kikuu cha Mzumbe kupitia mkataba wa makubaliano (MOU) unaotarajiwa kufanyiwa maboresho hivi karibuni.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa e-GA Eng. Benedict Ndomba, wakati wa kikao cha Pamoja kati ya e-GA na Chuo Kikuu cha Mzumbe kilichofanyika leo katika ofisi za e-GA jijini Dodoma, kwa ajili ya kujadili utekelezaji wa mkataba wa kwanza wa makubaliano (MOU).

Ndomba amesema kuwa, Mkataba wa kwanza wa makubaliano ulisainiwa Novemba 13, 2020 na umekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha mahusiano kati ya taasisi hizi mbili katika kuimarisha jitihada za Serikali Mtandao.

Naye Mkurugenzi wa TEHAMA Chuo Kikuu cha Mzumbe Dkt. Mohamed Ghasia, amesema kuwa chuo hicho kimepata mafanikio makubwa kutokana na mkataba huo ikiwa ni pamoja na kupata mafunzo mbalimbali kuhusu Serikali Mtandao, Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao, uwekaji wa taarifa katika tovuti , mfumo wa ofisi mtandao (e-office), barua pepe za serikali (GMS) pamoja na mafunzo ya usalama wa mtandao.

Pamoja na mafanikio hayo, Dkt. Ghasia pia alitaja baadhi ya changamoto zilizopo ambazo zinatakiwa kufanyiwa kazi kupitia MOU mpya itakayoandaliwa hivi karibuni ili kutatua changamoto hizo.

“Tunaona kuna pengo kubwa kati ya wahitimu wa vyuo vikuu na ujuzi unaohitajika katika soko la ajira, hivyo e-GA ikiwa ni mdau wetu mkubwa mtatusaidia sisi wa vyuo vikuu kufahamu maeneo tunayotakiwa kuboresha katika mitaala yetu ili kutengeneza vijana wanaoendana na soko la ajira”, amesema Ghasia.

Ameongeza kuwa, ni vema mifumo ya serikali ikawa endelevu na hivyo baadhi ya mifumo hiyo ikaingizwa katika mitaala ya vyuo vikuu ili kuwasaidia wanafunzi kuifahamu na kuweza kuitumia wanapoajiriwa katika taasisi za umma.

Ni vizuri pia wataalamu wa e-GA kuweka utaratibu wa kutembelea Vyuo Vikuu ili kutoa mafunzo kwa wanafunzi kuhusu mabadiliko ya teknolojia yaliyopo pamoja na mahitaji katika soko la ajira ili kuwatia hamasa katika masomo yao, amesema Dkt. Ghasia.

Mkataba mpya wa makubaliano kati ya e-GA na Chuo Kikuu cha Mzumbe unatarajiwa kuimarisha tafiti na bunifu za TEHAMA, kuandaa mikutano na vikao vya pamoja kati ya e-GA na Vyuo Vikuu pamoja na kuandaa eneo lenye mazingira wezeshi kwa wanafunzi kujifunza kwa vitendo.