emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

e-GA IMELETA MAGEUZI YA KIDIJITALI SERIKALINI: DKT. SAID MOHAMMED KATIBU MTENDAJI NECTA


e-GA IMELETA MAGEUZI YA KIDIJITALI SERIKALINI: DKT. SAID MOHAMMED KATIBU MTENDAJI NECTA


Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) Dkt. Said Mohammed, ameipongeza Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kwa jitihada inazofanya, katika mageuzi ya kidijitali Serikalini, jambo ambalo limechangia kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Dkt. Mohammed amesema hayo hivi karibuni ofisini kwake jijini Dar es Salaam, wakati alipofanya mahojiano maalum na mwandishi wetu kuhusu mchango wa e-GA katika mapinduzi ya kidijitali kwenye taasisi za umma.

Amesema kuwa, NECTA inajivunia sehemu kubwa ya mafanikio ya utoaji wa huduma katika kipindi cha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1973, kutokana na matumizi ya TEHAMA ambayo yamechagizwa na Mamlaka ya Seriikali Mtandao (e-GA).

“Kuanzishwa kwa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), kumechagiza matumizi ya TEHAMA katika Baraza la Taifa la Mitihani kwenye utoaji wa huduma mbalimbali, kwa watahiniwa ikiwemo hatua za awali za uendeshaji wa mitihani kama vile usajili na utoaji wa vyeti kwa watahiniwa”, amefafanua Dkt. Said.

Ameeleza kuwa, NECTA inafaidika na Mfumo wa Ofisi Mtandao (e-Office) ambao umesaidia katika utendaji wa shughuli mbalimbali za ndani za taasisi kwa kuongeza ufanisi, kwani mzunguko wa majalada hufanyika kwa urahisi na haraka na hivyo kurahisisha utoaji huduma kwa umma.

Ameongeza kuwa, NECTA imekuwa ikitumia Mfumo wa Kujisajili kupitia Mtandao (e-Service), Mfumo wa kuomba cheti mbadala kupitia mtandao na Mfumo wa kundaa matokeo na ripoti ili kusaidia watahaniwa kupata huduma kwa haraka mahali walipo.

Amebainisha kuwa, NECTA hushirikiana na e-GA katika ujezi wa mifumo ya kielektroniki ambayo hutumika katika utendaji kazi na utoaji wa huduma kwa wananchi kwa ufanisi na wakati .

“Sisi NECTA tumekuwa tukishirikiana na e-GA katika ujenzi wa mifumo lakini pia tunashirikiana katika kujengeana uwezo kupitia mafunzo mbalimbali yanayoandaliwa na e-GA yenye lengo la kutusaidia katika usimamizi na usalama wa taarifa (data) kwani, sisi NECTA tumekuwa tukizalisha na kuchakata taarifa nyingi kutokana na Idadi kubwa ya watahaniwa tunaokuwa nao”, amesisitiza Dkt. Said

Ameongeza kuwa, kutokana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia, Taasisi za Umma hazina budi kwenda sambamba na mabadiliko hayo kwa kuwekeza zaidi kwenye eneo la TEHAMA na kuimarisha usalama wa taarifa mtandaoni, nyaraka na mifumo kwa ujumla.

“Ni lazima sisi kama watendaji tuwe tayari kubadilika na kuendana na kasi hiyo kwa kufanya uwekezaji zaidi kwenye TEHAMA na kuangalia usalama wake” Amesema Dkt. Mohammed

Ameongeza kuwa, NECTA imedhamiria kuhakikisha huduma zote zinatolewa kupitia mtandao ikiwemo ufundishaji (e- Teaching na e-Learning) pamoja na utahini kupitia mtandao (e assessment).

“Kutokana na mafanikio tunayoyapata kupitia e-GA, NECTA itandeleza ushirikiano mzuri uliopo ili tuweze kufikia malengo ya taasisi na kurahisisha utoaji wa huduma za umma kwa wepesi na ufanisi zaidi”, amesema Dkt. Said.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Mhandisi, Benedict Ndomba amepongeza jitihada zinazofanywa na NECTA katika matumizi ya TEHAMA kwenye utendaji kazi wake na utoaji wa huduma kwa wananchi.

Ndomba amesema kuwa, NECTA ni moja kati ya taasisi zilizofanya mageuzi makubwa katika utoaji wa huduma kidijitali na hivyo kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma hizo.

Ndomba ametoa rai kwa Taasisi za Umma kuwekeza katika TEHAMA kutumia mifumo ya kielektroniki katika utoaji wa huduma kwa wananchi ili kuongeza tija na ufanisi katika utendaji kazi.