emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

DKT. MPANGO AZITAKA TAASISI ZA UMMA KUJIUNGA NA GOVESB


DKT. MPANGO AZITAKA TAASISI ZA UMMA KUJIUNGA NA GOVESB


MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Philip Mpango, amezielekeza taasisi za umma kuwasiliana na kubadilishana taarifa kidijitali, ili kurahisisha utendaji kazi katika taasisi zao na utoaji wa huduma za Serikali kwa wananchi kwa urahisi na gharama nafuu zaidi.

Dkt. Mpango amesema hayo leo, wakati akifungua Kikao Kazi cha 5 cha Serikali Mtandao, kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC) jijini Arusha, na kuhudhuriwa na takribani wadau 1,500 wakiwemo Maafisa Masuuli, Wakurugenzi na Wakuu wa Vitengo vya TEHAMA, Maafisa TEHAMA na watumiaji wengine wa mifumo ya TEHAMA kutoka katika Taasisi, Halmashauri na Mashirika mbalimbali ya Umma.

Dkt. Mpango amesisitiza kuwa, ili kuleta mapinduzi ya kidijitali Serikalini na matumizi endelevu ya TEHAMA, Taasisi za Umma zinapaswa kujiunga na Mfumo Mkuu wa Ubadilishanaji Taarifa Serikalini (Government Enterprise Service Bus - GoVESB).

Aidha, Dkt. Mpango amezitaka Taasisi za Umma, ambazo hazijahuisha taratibu za utendaji kazi wake ‘Business processes’, kuhakikisha zinafanya hivyo ili, kuweza kujenga Mifumo inayowasiliana na kubadilishana taarifa kwa urahisi.

“Ili Taasisi za Umma ziweze kuwasiliana na kubadilishana taarifa, ni lazima taratibu za utendaji kazi wa taasisi ‘Business processes’ ziandaliwe na kuwekwa kwenye maandishi, hivyo ni lazima kuhakikisha kila taasisi inatekeleza agizo hili” amesisitiza Dkt. Mpango.

Amebainisha kuwa, katika kuhakikisha mifumo ya afya inawasiliana na kubadilishana taarifa, Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), tayari imendaa taratibu za utendaji zilizoboreshwa, ikiwa ni kuelekea hatua ya kuwa na Mfumo utakaoweza kutumiwa na Hospitali nyingi kwa pamoja.

“Tunategemea kuona mgonjwa anayetibiwa Hospitali ya Mount Meru hapa Arusha anapokwenda Muhimbili, Daktari aweze kuona taarifa za historia ya mgonjwa moja kwa moja kutoka Hospitali ya Mount Meru kupitia Mfumo”, amesisitiza Dkt. Mpango.

Aidha, Dkt. Mpango amezitaka sekta nyingine kuiga mfano wa Wizara ya Afya, kwa kuhuisha taratibu zake ili kuchochea mageuzi ya kidijitali katika utendaji kazi na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi kwa haraka na gharama nafuu.

Vilevile, Dkt. Mpango ameipongeza e-GA kwa kutekeleza agizo la Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluh Hassan, kwa kusanifu na kujenga Mfumo wa GoVESB, ambao umeleta matokeo chanya katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya haki jinai.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene, amesema kuwa, Serikali imewekeza katika TEHAMA, kwakuwa ni nyenzo muhimu katika kuleta utawala bora na kuongeza ufanisi Serikalini, ili kurahisisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Mhe. Waziri amesema matumizi ya TEHAMA Serikalini yamesaidia kwa kiasi kikubwa utendaji kazi wa shughuli nyingi za Serikali hivyo kuongeza ufanisi katika kuwahudumia wananchi kwa wakati.

Kikao Kazi cha Tano cha Serikali Mtandao kinaongozwa na kauli mbiu isemayo, “Jitihada na ubunifu wa Serikali mtandao kwa utoaji huduma za umma kwa ufanisi” ili kuchochea matumizi ya bunifu mbalimbali za TEHAMA, itakayosaidia utoaji wa huduma za umma kwa ufanisi