emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

WAKAGUZI WA NDANI WA HALMASHAURI WAPEWA MAFUNZO YA UKAGUZI WA MIFUMO YA TEHAMA


WAKAGUZI WA NDANI WA HALMASHAURI WAPEWA MAFUNZO YA UKAGUZI WA MIFUMO YA TEHAMA


Mamlaka ya Serikali Mtandao e-GA imewataka Wakaguzi wa ndani wa Halmashauri na Tawala za Mikoa kuzingatia sheria na miongozo ya Serikali Mtandao, wakati wa ukaguzi wa Mifumo ya TEHAMA katika Taasisi zao ili kupunguza hoja za ukaguzi.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa e-GA Mhandisi. Benedict Ndomba, wakati wa Mafunzo ya siku tano (05) ya kuwajengea uwezo Wakaguzi wa Ndani wa halmashauri na Tawala za Mikoa ili waweze kukagua Mifumo ya TEHAMA inayotumika katika Taasisi zao.

Ndomba alieleza kuwa, mafunzo hayo ni utekelezaji wa moja ya mapendekezo yaliyotolewa na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) ya kuitaka e-GA kushirikiana na Taasisi za Umma kuandaa mpango mkakati na utekelezaji wake katika kushughulikia ukaguzi wa Mifumo ya TEHAMA.

“Mafunzo haya tumeyandaa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali (IAG) ili kuwawezesha Wakaguzi wa Ndani wa halmashauri na Tawala za Mikoa, kufanya ufuatiliaji wa miradi ya TEHAMA katika Taasisi zenu”, alisema Ndomba.

Aidha, Ndomba aliwataka Wakaguzi wa Ndani kufanya kazi kwa karibu na e-GA na kuwasilisha changamoto zozote watakazokutana nazo wakati wa utekelezaji wa majukumu yao katika ukaguzi wa miradi ya TEHAMA na kuahidi kuzifanyia kazi kwa wakati.

“Sio vizuri kuwa na hoja za kiukaguzi hasa zile ambazo zinaweza kupatiwa suluhu kama vile, hoja ya kutokuwepo kwa sera ya TEHAMA katika Taasisi kwakuwa tayari miongozo imekwishaandaliwa na e-GA, hivyo kupitia mafunzo haya mtaweza kubaini namna gani mnaweza kuondokana na hoja za aina hiyo”, alisisitiza Ndomba.

Ndomba aliongeza kuwa, kupitia mafunzo hayo, wataalamu hao wataweza kubaini mapungufu yanayojitokeza katika miradi na mifumo ya TEHAMA katika taasisi zao na kuweza kushauri namna ya kuboresha.

Ndomba aliahidi kuwa, Mamlaka ya Serikali Mtandao itaendelea kuwajengea uwezo wataalamu hao kutokana na mabadiliko ya Teknolojia yanayoibuka kila mara.

Kwa upande wake mwakilishi wa washiriki wa mafunzo hayo Adeline Komba, alishukuru e-GA na Ofisi ya IAG kwa kufanikisha mafunzo hayo, kwani Wakaguzi wa Ndani wamekuwa wakiyahitaji mafunzo hayo kwa muda mrefu.

“Uelewa wa Wakaguzi wa Ndani si mkubwa na wamekuwa wa mwisho kupewa mafunzo hayo hivyo nashauri wapewe mafunzo mapema wakati wa ujenzi wa Mifumo”, alisema Komba.

Vilevile Komba aliishauri e-GA kuwa na dawati maalum la kushughulikia changamoto mbalimbalimbali zinazojitokeza ili ziweze kutatuliwa kwa wakati, ushauri ambao ulipokelewa na Mkurugenzi Mkuu wa e-GA, Mhandisi Benedict Ndomba na kuahidi kutekelezwa kupitia dawati la msaada ‘helpdesk’.

Mafunzo hayo yamewakutanisha jumla ya washiriki 133 kutoka katika halmashauri na Tawala za Mikoa (13).