WAZIRI MKUU wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), amesema kuwa matumizi ya Mfumo wa Kielektroniki wa Baraza la Mawaziri (e-Cabinet), unalenga kurahisisha utendaji kazi wa baraza hilo sambamba na kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Mhe. Majaliwa amesema hayo Novemba 11 mwaka huu, wakati akifunga Mkutano wa Kazi wa Mawaziri na Naibu Mawaziri, kuhusu matumizi ya mfumo wa e-CABINET, uliofanyika katika ukumbi wa Hazina jijini Dodoma
Amebainisha kuwa, mfumo huo utasaidia kupunguza matumizi ya karatasi katika vikao vya Serikali, hususan Baraza la Mawaziri na hivyo kuokoa fedha za Serikali zilizokuwa zikitumika katika ununuzi wa karatasi hizo.
"Mfumo huu utaturahisishia utendaji kazi na kuweza kuwahudumia wananchi kwa wakati na kutatua changamoto mbalimbali zikiwemo kuchelewa kwa taarifa na hatari ya upotevu wa taarifa muhimu", amesema Mhe. Majaliwa.
Ameongeza kuwa, ujenzi wa mfumo huo unatokana na jitihada za Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika kuleta mageuzi ya kidijitali Serikalini kupitia Mamlaka ya Serikali Mtadao (e-GA) .
Amesema kwa, kutokana na jitihada na nia thabiti ya Mhe. Rais katika matumizi ya teknolojia Serikalini, Tanzania imeweza kupiga hatua kubwa katika matumizi ya teknolojia na kuongoza katika ukanda wa Afrika Mashariki.
“Matokeo ya utafiti wa mwaka 2022 uliofanywa na Benki ya Dunìa kuhusu ulinganifu baina ya nchi katika muktadha wa Ukomavu wa Matumizi ya Teknolojia Serikalini (Government Technical Maturity Index), nchi yetu ilishika nafasi ya tatu (3) ikilinganishwa na nchi nyingine Barani Afrika na hii ni kutokana na jitihada za Mhe. Rais katika uwekezaji kwenye matumizi ya teknolojia", amesema Mhe. Majaliwa.
Ameongeza kuwa, matumizi ya mfumo huo ni sehemu ya juhudi za Serikali katika kuhakikisha kwamba, Mawaziri na watumishi wa umma wanakuwa na ujuzi wa kisasa wa uendeshaji wa shughuli za Serikali na utumishi kwa ujumla kupitia TEHAMA.
Aidha, amefafanua kuwa uanzishwaji wa mfumo huo wa e-Cabinet, ni utekelezaji wa Ibara za 102 na 103 za Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020 zinazoelekeza Serikali kuhakikisha kuwa sayansi, teknolojia na ubunifu vinatumika kikamilifu katika kuendesha sekta za kukuza uchumi kwa lengo la kufikia uchumi wa hadhi ya kipato cha kati ambao ni shindani, jumuishi na unaoongozwa na viwanda.
Kwa Upande wake, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko (Mb) amewapongeza wataalam kutoka Mamlaka ya Serikali Mtandao kwa kufanikisha mafunzo hayo, na kuwataka kuendelea na jitihada mbalimbali za ujenzi wa Serikali ya Kidijiti.
Naye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (Mb), amesema kuwa mafunzo hayo ni mwendelezo wa mpango wa Serikali kwenda kwenye matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa Baraza La Mawaziri (e-CABINET).
Amebainisha kuwa, mchakato wa ujenzi wa mfumo huo ulikuwa ni wa muda mrefu kupitia wataalam wa e-GA, na kuahidi kuendelea kuisimamia vema Mamlaka hiyo ili kuhakiisha matumizi ya TEHAMA Serikalini yanaimarika katika sekta zote.