emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Tovuti ni Muhimu Kwa Huduma Mtandao


Tovuti ni Muhimu Kwa Huduma Mtandao


Taasisi za umma zimetakiwa kuwa na tovuti zitakazosaidia wananchi kupata kwa urahisi taarifa zinazohusu shughuli na huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi hizo.

Wito huo umetolewa na Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali Mtandao Dkt. Jabiri Bakari wakati akizungumza na  wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari aliowakaribisha katika ofisi za Wakala ili kuwaeleza utekelezaji wa serikali mtandao unaosimamiwa na Wakala yake, Mei 17, 2016. 

“Tovuti za Serikali zinatakiwa kuwa kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza na  mwananchi anapofungua tovuti hizo lugha itakayoonekana kwanza iwe ni  Kiswahili na muda wowote mwananchi huyo anaweza kubadili kwenda kwenye lugha ya Kiingereza”, amesema Dkt Bakari. 

Dkt. Bakari amesema kuwa Wakala imetoa miongozo ya  kusimamia na kuendesha tovuti hizo. Mwongozo huo unapatikana kwenye tovuti ya Wakala www.ega.go.tz sehemu ya Miongozo na Viwango.

Akizungumzia mafanikio ya Wakala amesema Wakala imetengeneza mifumo mbalimbali na kuweka miundombinu ya kuwezesha taasisi za umma kutumia Tehama katika utoaji wa  huduma kwa wananchi. 

“Tovuti Kuu ya Serikali ni zao la kwanza la Wakala na ilibuniwa na kusanifiwa na wataalam wetu wa ndani. Katika tovuti hiyo ambayo pia ni mfumo, ina taarifa za baadhi ya taasisi za umma, sekta mbalimbali na huduma zake pamoja na balozi zilizoko nchini na zile za kwetu zilizoko nje ya nchi”, amesema Dkt. Bakari. 

Vilevile, amesema kuwa tovuti hiyo ina sehemu ya Nifanyeje ambayo ina maelezo na maelekezo ya namna ya kupata huduma za Serikali zinazotolewa na baadhi ya taasisi za umma. Aidha, mwananchi anaweza kuona taasisi husika kijiografia kwa kutumia mfumo wa ramani wa Google.

Mfumo mwingine uliotengenezwa na Wakala, amesema mkuu huyo ni Tovuti Kuu ya Ajira ambayo humwezesha mwananchi kuona ajira mbalimbali zinazotangazwa na Serikali ambapo muombaji wa ajira anaweza kutuma  wasifu wake  kwa njia ya mtandao na  nafasi zinapotangazwa zenye kuhitaji mtu mwenye sifa hizo, anapata  ujumbe moja kwa moja kupitia simu yake ya mkononi na kuombwa kuthibitisha kama anahitaji nafasi hiyo ili mfumo upeleke wasifu wake kwenye orodha ya waombaji.

Pia, Wakala imesanifu Tovuti Kuu ya Takwimu Huria inayoonesha takwimu mbalimbali za sekta tatu zilizopewa kipaumbele, sekta hizo ni Elimu, Afya na Maji. Vilevile Dkt. Bakari amesema Wakala imetengeneza Tovuti Rasmi ya Mwananchi ambayo inamwezesha mwananchi kuwasilisha maswali na hoja mbalimbali ambazo hutolewa majibu kwa wakati na Serikali.

Pamoja na tovuti hizo Kuu, baadhi ya wizara, mikoa, wilaya, halmashauri na taasisi zimetengenezewa  tovuti na Wakala kwa madhumuni hayo.

Naye Meneja wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano wa Wakala hiyo Bi. Suzan Mshakangoto aliwataarifu wahariri hao kuhusu jitihada   mbalimbali zinatekelezwa na  Wakala ili kuwezesha taasisi za umma kutoa huduma zao kwa njia ya mtandao kwa kuongeza uwezo wa wataalam wa Tehama  kwa kuwapa maarifa na ustadi wa kubuni, kutengeneza na kutumia mifumo tumizi, ikiwemo miundombinu  inayowezesha utoaji wa huduma kwa njia ya kompyuta au vitumi vingine. 

“Tumetoa Mafunzo ya Usimamizi na Ujenzi wa Mtandao wa Mawasiliano Serikalini na Usalama wa Mtandao kwa taasisi za umma 149 wakiwemo Maofisa TEHAMA 226, Mafunzo ya Uendeshaji wa Vituo vya Data kwa Taasisi za umma 91 wakiwemo Maofisa TEHAMA 162, Mafunzo ya Usimamizi wa Mfumo wa Barua Pepe Serikalini yametolewa kwa taasisi 157 pamoja na Mafunzo ya usimamizi wa taarifa tovuti za serikali yametolewa kwa taasisi 71. Mafunzo ya uwekaji taarifa katika tovuti kuu yametolewa kwa taasisi 86 na Mafunzo hayo yanaendelea kutolewa kwa kila taasisi ambayo inatengenezewa Tovuti na Wakala”, alifafanua Bi. Mshakangoto.

Lengo kuu la jitihada zote hizo, anasema meneja huyo ni kuziwezesha Taasisi hizo kutumia TEHAMA katika majukumu yao ili kuongeza ufanisi na  uwajibikaji wakati huo huo kumwezesha mwananchi kupata huduma bora, fanisi na zenye gharama nafuu.