Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali Mtandao (eGA) Dkt. Jabiri Bakari amewataka Maafisa Habari na Wachambuzi wa Mifumo ya kompyuta wa Mkoa na Halmashauri za Mkoa wa Mtwara kuhamasisha watumishi wa Mkoa na Halmashauri zake kutumia Mfumo wa Barua Pepe Serikalini (Government Mailing System) ili kutumia mfumo wa mawasiliano ambao ni salama na wa uhakika kati ya watumishi na taasisi za Serikali.
Dkt. Bakari amesema hayo wakati akifungua mafunzo ya matumizi ya mfumo wa Barua Pepe Serikalini kwa Maofisa hao yanayofanyika kwa muda wa siku mbili Juni 1 na 2, 2015 katika ukumbi wa mikutano wa Wakala uliopo Jijini Dar es salaam.
Aliongeza kuwa mfumo huu unafanya kazi kwa ufanisi na unazidi kuboreshwa siku hadi siku ili kukidhi mahitaji ya watumiaji. Pia alisisitiza kuwa Mfumo huu ni matokeo ya utafiti wa kina wa miundombinu ya mifumo ya barua pepe kwenye taasisi za Serikali uliobainisha kuwapo na matatizo ya jumla ya mawasiliano katika mifumo isiyo na uhakika katika upatikanaji, iliyotawanyika na isiyo salama.
Aidha, Dkt. Bakari amewahimiza maofisa kuhakikisha kuwa tovuti zao zina maudhui yatakayowasaidia wananchi kupata taarifa za manufaa wanazohitaji kwa urahisi.
“Wawezesheni wananchi kutumia muda mfupi kupata huduma kwa kuweka taarifa za awali mtandaoni, hasa mkijibu maswali ya nini wanatakiwa kufanya na nani anahusika ili kupata huduma” alisema Dkt. Bakari.
Aliongeza Serikali Mtandao ina hatua tano ambazo zinaendelea kuzingatiwa na hatua ya mwisho inawawezesha wananchi kujaza fomu ya huduma wanayoitaka na kupata huduma hiyo kwa njia ya mtandao hali itakayosaidia kuondoa urasimu.
Dkt. Bakari aliwataka wataalamu hao kuhakikisha wanaonyesha huduma muhimu za kijamii pamoja na shughuli nyingine muhimu zinazofanywa katika Mkoa na Halmashauri zao ili kuwawezesha wananchi kupata ufahamu wa jinsi Serikali inavyotekeleza majukumu yake.
Naye Mkurugenzi wa Usimamizi wa TEHAMA Bw. Benedict Ndomba ameongeza kwa kuwataka maofisa hao kuhakikisha wanarudi katika sehemu zao za kazi wakiwa wametatua matatizo ya kitalaamu yaliyopo katika tovuti hizo.