emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Watumishi wa TBA wapewa Mafunzo


Watumishi wa TBA wapewa Mafunzo


Mtendaji Mkuu wa Wakala Dkt. Jabiri Bakari amewataka washiriki wa mafunzo kutoka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kuwasikiliza wawezeshaji wa mafunzo kwa makini ili kupata uelewa mpana wa jinsi ya kutumia mfumo wa Usimamizi wa Rasilimali za Serikali (Government Real Estate Management System) ambao ni mahususi kwa Wakala wa Majengo Tanzania.

Alisema hayo wakati alipokuwa akifungua rasmi mafunzo ya siku tano ya jinsi ya kutumia mfumo huo yanayoendeshwa na Wakala ya Serikali Mtandao katika ukumbi wa mafunzo wa Wakala hiyo.

Dkt. Bakari ameongeza kuwa mfumo huo umetengezwa ili kuisadia TBA katikakusimamia rasilimali, miradi, mambo ya kiutendaji na kuharakisha upatikanaji wa huduma kwa umma kwa haraka na kwa gharama nafuu.

“Baadhi ya taasisi za umma zimeendelea kutoa huduma kwa utaratibu wa kawaida (manual) kwa kuwa hawaelewi vizuri jinsi ya kutumia mifumo inayotengenezwa na kampuni mbalimbali, ingawa wataalam wake hupewa fursa ya kwenda kupata mafunzo” Alisema Dkt. Bakari.

Aidha, amesema kuwa washiriki wa mafunzo hayo wanapaswa kuufahamu mfumo huo kwa undani zaidi na kisha baada ya mafunzo watoe maoni ya jinsi ya kuuboresha kabla haujaanza kutumika.

Naye mratibu wa mradi huo Bw. Eden Mathew amewahakikishia watumishi hao wa TBA kuwa, maoni watakayotoa yatafanyiwa kazi kwa haraka ili kwenda sambamba na muda uliopangwa.

“Watalaam wetu wako tayari kuweka katika mfumo maoni yenu ili baada ya muda wa mafunzo, mfumo huo uanze kufanya kazi mara moja” Alisema Bw. Mathew.