Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Dodoma imefurahishwa na huduma mbalimbali zinazotolewa na Wakala katika kuziwezesha taasisi za Umma kutoa huduma bora kwa wananchi na kwa wakati.
Hayo yamesemwa na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa huo Bw,Deogratias Yinza katika kikao cha pamoja kati ya Wakala na Menejimenti ya Ofisi hiyo Juni 26, 2015.
Wajumbe wa Menejimenti hiyo walitaka kufahamu jitihada za Serikali Mtandao katika kukabiliana na wavamizi wa mitandao ambapo Bw. Ndomba alisema Wakala ina wataalamu wa kushughulikia masuala ya usalama wa mitandao, pia Wakala inatoa mafunzo mbalimbali kwa watumishi wa Umma ili kudhibiti tatizo hilo.
“Wakala inajitahidi kuhakikisha mitambo yote inayotumika ihifadhiwe nchini Tanzania na tunashukuru hadi sasa hatujapata uvamizi wa mtandao ila ni muhimu kuwa makini katika matumizi ya mitandao”, alisema Ndomba.
Akizungumza katika kikao hicho, Meneja wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano wa Wakala Bi.Suzan Mshakangoto alisema ni muhimu kwa Ofisi hiyo kuweza kusoma taarifa mbalimbali zinazopatikana kwenye Tovuti Kuu ya Serikali kwa kuwa ina taarifa zote muhimu za Serikali ikiwemo Sheria, Miongozo, Gazeti la Serikali na taarifa nyinginezo.
Wakala ya Serikali Mtandao inatembelea taasisi za Serikali kwa lengo la kujitangaza na kuzinadi huduma mbalimbali zinazotolewa ili kuziwezesha taasisi hizo ziweze kutoa huduma bora kwa wananchi.