emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Taasisi Za Umma Zashauriwa Kufuata Miongozo Na Viwango Vya TEHAMA


Taasisi Za Umma Zashauriwa Kufuata Miongozo Na Viwango Vya TEHAMA


Wakala ya Serikali Mtandao imezishauri Wizara, Idara zinazojitegemea, Sekreterieti za Mikoa, Wakala za Serikali/Mamlaka, Bodi, Tume, Mabaraza, Mifuko, Mashirika ya umma na Mamlaka za Serikali za Mitaa kufuata miongozo na viwango vilivyotolewa katika uanzishaji na usimamizi wa mifumo ya Tehama Serikalini.

Hayo yamesemwa na Meneja Habari, Elimu na Mawasiliano wa Wakala Bi. Suzan Mshakangoto alipozungumza na waandishi wa habari Machi 3, 2015 katika ukumbi wa Habari Maelezo jijini Dar es Salaa.

Bi. Mshakangoto alisema Miongozo na viwango hivyo vinalenga kuziwezesha taasisi za umma kujenga mifumo inayoendana na mahitaji halisi ya taasisi husika na kuepuka mifumo inayojengwa kwa shinikizo la wafanyabiashara, wafadhili au kwa matakwa ya mtu binafsi.

“kwa kutumia miongozo na viwango vya sasa, Serikali itakuwa na uwezo wa kuepuka urudufu wa mifumo na kupunguza gharama kubwa za uendeshaji na kuwa na mifumo endelevu na yenye gharama halisi na inayofuata viwango vya Usalama katika kulinda taarifa na data za Serikali”, alifafanua Bi. Mshakangoto

Naye Mkurugenzi wa Usimamizi wa Huduma za TEHAMA Bw. Benedict Ndomba alisema, taasisi za umma zinashauriwa kuwasilisha maandiko ya mifumo mipya ya TEHAMA ili iweze kuthibitishwa iwapo imefuata miongozo na viwango vilivyowekwa kabla ya kujengwa na kusakinishwa.

Aliongeza kuwa, taasisi hizo zinatakiwa kujaza taarifa za mifumo au miradi ya TEHAMA iliyopo katika mfumo wa kukusanya na kutunza taarifa za miradi ya TEHAMA Serikalini unaopatikana katika anuani ya http://gip.ega.go.tz.

“Miongozo na viwango vitapitiwa mara kwa mara na kuchapishwa kulingana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia, mahitaji ya shughuli na matakwa ya Serikali. Pia, Viwango na Miongozo hii inapatikana katika tovuti ya Wakala ya Serikali Mtandao www.ega.go.tz  sehemu ya miongozo na viwango”,alieleza Bw. Ndomba.

Pia, aliwatahadharisha wafanyabiashara wanaojihusisha na miradi au utengenezaji wa mifumo ya TEHAMA Serikalini kufuata miongozo na viwango katika kubaini mahitaji halisi ya Serikali ili kujenga mifumo ya TEHAMA endelevu na inayoleta tija kwa umma.

Wakala ya Serikali Mtandao (e-Government Agency) ni Taasisi ya Serikali iliyoanzishwa mwaka 2012 kwa sheria ya Wakala za Serikali Na. 30, Sura ya 245 ya mwaka 1997. Wakala hii ina majukumu na mamlaka ya kuratibu, kusimamia na kukuza jitihada za Serikali Mtandao nchini Tanzania.