emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Taasisi za Umma Zatakiwa Kuhuisha Taarifa


Taasisi za Umma Zatakiwa Kuhuisha Taarifa


Serikali imeziagiza taasisi zote za umma kuhuisha taarifa zilizomo kwenye tovuti zao, ikiwemo Tovuti Kuu ya Serikali (www.tanzania.go.tz) na kupokea na kujibu hoja za wananchi katika Tovuti ya Wananchi (www.wananchi.go.tz) kwa wakati ili kuwapatia wananchi huduma bora.

Agizo hilo limetolewa  na Msemaji Mkuu wa Serikali, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Bw. Hassan Abbas wakati wa mkutano na waandishi wa vyombo vya habari uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Wakala ya Serikali Mtandao, Oktoba 05, 2016.

“Naziagiza taasisi zote za umma kuanzia sasa mpaka ifikapo mwisho wa mwezi huu wa kumi kukamilisha zoezi zima la kuhuisha taarifa zao. Maofisa Habari na TEHAMA waanze mara moja kazi hii ili wananchi wapate taarifa mbalimbali za Serikali ikiwa ni pamoja na huduma zinazotolewa na taasisi hizo”, alisisitiza Bw. Abbas.

Ameongeza kuwa, tovuti za Serikali zina changamoto ya kimaudhui yaani kuwa na taarifa zilizopitwa na wakati jambo ambalo linachangiwa na baadhi ya maofisa habari na TEHAMA kufanya kazi kwa mazoea kwa kutoona umuhimu wa kuweka taarifa kwa wakati .

Amesema kuwa, changamoto nyingine ni ya kiusanifu ambapo baadhi ya taasisi zinaonekana kusanifu tovuti zao kinyume na mwongozo wa kuendesha na kusimamia tovuti za Serikali uliotolewa mwaka 2014 na hivyo kusababisha tovuti hizo kuwa tofauti na zile zilizofuata taratibu zilizowekwa.

“Ifikapo mwisho wa mwezi wa kumi, taasisi yoyote ya umma ikigundulika kuwa haikufuata  agizo hili itachukuliwa  hatua stahiki itakayotangazwa hapo baadae. Jukumu la  kufuatilia suala hili linafanywa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Wakala ya Serikali Mtandao na ni kazi endelevu”, alisisitiza Bw. Abbas.

 Naye Meneja wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa Wakala ya Serikali Mtandao Bi. Suzan Mshakangoto amesema Serikali ina taasisi 498 ambapo kati ya hizo, taasisi 200 pekee ndio zenye tovuti, ambapo Wakala imetengeneza tovuti 80 kati ya hizo 200.

“Nazishauri taasisi ambazo zina tovuti ambazo hazijafuata mwongozo wa kusimamia tovuti za Serikali kutembelea tovuti ya Wakala ya Serikali Mtandao inayopatikana kwa anwani ya www.ega.go.tz sehemu ya miongozo na viwango ili wausome mwongozo huo; hali kadhalika wakandarasi wanaotengeneza tovuti za Serikali, ni vema wakazingatia mwongozo huo”, alisema Bi. Mshakangoto.

Aliongeza kuwa, Mwongozo huo unalenga kutatua changamoto za tovuti hizo na kuziwezesha taasisi za umma kuandaa tovuti zenye mwonekano unaoshabihiana na alama za taifa, utakaokidhi mahitaji ya wadau na pia kuwapa urahisi wa kuvinjari wakati wa kutafuta taarifa au kupata huduma. Pia mwongozo huo, alisema Meneja huyo, ni muhimu kwani unatoa maelekezo ya kuongeza ubora na usalama wa tovuti za Taasisi za umma na kutoa uelewa wa kutosha kwa mtumiaji kuhusu taarifa na huduma za Serikali.