emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Simu za Mkononi Kurahisisha Huduma za Serikali kwa Wananchi


Simu za Mkononi Kurahisisha Huduma za Serikali kwa Wananchi


Maafisa TEHAMA na Maafisa Biashara wa taasisi mbalimbali za umma wamehimizwa kujiunga na kutumia Mfumo wa Huduma za Serikali kwa Simu za Mkononi ili waweze  kutoa huduma bora kwa wananchi kwa urahisi na  haraka.

Akifungua mafunzo ya Huduma za Serikali Kupitia Simu za Mkononi kwa maofisa wa taasisi za Serikali, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Huduma za TEHAMA wa Wakala ya Serikali Mtandao, Bw.Benedict Ndomba amesema kuwa simu za mkononi zitawezesha maafisa hao kutumia weledi na ubunifu katika kutoa huduma kwa wananchi.

“Mafunzo haya mnayopata yawabadilishe na kuwasaidia kufanya kazi zenu kwa weledi na muwe wabunifu zaidi ili wale wote mnaohudumia waone furaha ya kupata huduma za Serikali kwa urahisi viganjani mwao kupitia simu zao na sio wahangaike na kwenda umbali mrefu kutafuta huduma kwenye ofisi zenu”, alisema Bw. Ndomba.

 Aidha, Mkurugenzi huyo alielezea kuwa kupitia huduma ya Serikali kupitia simu za mkononi wananchi wanaweza kulipia malipo mbalimbali ya Serikali, kujua bei za mafuta, kupata taarifa za ajira mpya pamoja na huduma nyingine nyingi zinazotolewa na Serikali.

Pia Bw. Ndomba aliwashauri maofisa hao watakaporudi katika maeneo yao ya kazi wawahimize wakuu wao wa taasisi waanze kutumia huduma mbalimbali zinazotolewa na Wakala, ikiwemo Huduma za Serikali Kwa Simu za Mkononi ili kuweza kurahisisha utendaji kazi na kuwafikia walengwa wa huduma kwa urahisi.

Naye Bi. Joan Msangi, mhudumia wateja wa Bohari Kuu ya Dawa Tanzania (MSD) amesema kuwa mafunzo hayo yana umuhimu mkubwa kwa taasisi yao na kupitia huduma hiyo ya Serikali kwa Simu za Mkononi itawasaidia kuwafikia wateja wao wengi kwa wakati na itawaweka karibu zaidi.

Vile vile Bi. Msangi amesema kuwa elimu aliyoipata imekuja wakati mwafaka kwani MSD ipo kwenye mchakato wa mwisho wa kufungua kituo cha huduma kwa wateja, hivyo kupitia huduma hii taasisi itahudumia na kuwafikia wateja wengi kupitia mawasiliano kwani asilimia kubwa ya wadau wa MSD si watumiaji wazuri wa barua pepe bali ni watumiaji wazuri wa simu za mkononi.

Pia Bi. Joan aliishauri  Wakala iwe inatoa mafunzo ya huduma zake nyingine mara kwa mara ili waweze kuzifahamu na kuona umuhimu wa kuzitumia na  itasaidia kwa watumishi wa Serikali kufanya kazi kwa kitaalamu zaidi.

Aidha, Afisa TEHAMA wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania, Bw. Yahaya Abdallah ameishauri Wakala iwe inatoa mafunzo kwa wakuu wa taasisi mbalimbali za Serikali ili wafahamu na waone umuhimu wa huduma mbalimbali zitolewazo na Wakala na kuamua kujiunga na huduma hizo.

 

Mafunzo hayo ya awamu ya pili kwa taasisi zipatazo 13 za Serikali ya jinsi ya kuboresha utoaji wa Huduma za Serikali kwa kutumia Simu za Mkononi yalianza rasmi Oktoba 9 na kukamilika Oktoba 13, 2017 katika ofisi za Wakala jijini Dar es Salaam.