Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Mhe. Angella Kairuki amewataka wataalam wa TEHAMA kushirikiana na Wakala ya Serikali Mtandao ili kupata ushauri wa kitaalam katika utekelezaji wa masuala mbalimbali ya TEHAMA katika taasisi zao.
Waziri Kairuki amesema hayo wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa maofisa TEHAMA yanayoendeshwa na watalaam kutoka UCC ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mjini DODOMA yaliyoanza Januari 19, 2016.
Aidha, amewaagiza maofisa hao kusimamia matumizi ya barua pepe za Serikali katika mawasiliano ya Serikali kwa Watumishi wa taasisi zao pamoja na kubuni mifumo mbalimbali ya TEHAMA kufuatana na majukumu ya taasisi husika ili kuboresha utendaji kazi na utoaji huduma.
“Mkirudi katika vituo vyenu vya kazi, hakikisheni mnaratibu utekelezaji wa miongozo na nyaraka mbalimbali za TEHAMA zilizokwishatolewa na Serikali na ambazo zinapatikana kwenye Tovuti ya Ofisi ya Rais-UTUMISHI (www.utumishi.go.tz) pamoja na ile ya Wakala ya Serikali Mtandao (http://ega.go.tz/). Pia, mnatakiwa kuwezesha kikamilifu utekelezaji wa mifumo, Tovuti na Miundombinu ya TEHAMA ilizokwishawekwa kwenye taasisi zenu katika kuboresha utendaji kazi na utoaji wa huduma”, alisisitiza Waziri Kairuki.
Aidha Waziri kairuki ameiagiza Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma kufanya tathmini ya matumizi ya ujuzi utakaopatikana katika mafunzo hasa ubunifu utakofanyika kufuatia mafunzo hayo.
Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali Mtandao, Dkt. Jabiri Bakari alimweleza Waziri huyo kuwa maeneo makuu ya mafunzo hayo ni Uendelezaji wa Mifumo, Cloud Computing, Uendelevu wa Biashara , Ukaguzi wa Mifumo ya Taarifa, Usimamizi wa Hazina Data, Usanifishaji wa Shughuli, Utengenezaji,Usimamizi na Uendeshaji wa Tovuti na Mifumo Tumizi ,Usimamizi na Uendeshaji wa Mtandao, Uendeshaji wa seva na Usimamizi pamoja na Vitumi vya Mikononi.
“Mafunzo haya yanajumuisha maofisa TEHAMA 210 waliochaguliwa kutoka Wizara , Idara zinazojitegemea Wakala za Serikali pamoja na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Mafunzo haya yatafanyika kwa awamu kumi (10) kuanzia Januari 19 hadi Juni 3, 2016 katika vituo vya UCC Dar es Salaam na Dodoma”, alisema Dkt. Bakari.