emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

MUHAS wahuisha tovuti yao


MUHAS wahuisha tovuti yao


“Tumeamua kuiboresha tovuti yetu ili iwe nzuri zaidi na yenye taarifa zilizopangiliwa vizuri. Naamini tovuti hii itasaidia kupandisha hadhi ya chuo chetu dhidi ya vyuo vikuu vingine ukizingatia kuwa sasa huduma na shughuli mbalimbali zinazofanyika chuoni kwetu zimewekwa kwa mpangilio mzuri zaidi na wenye kueleweka”, amesema Ofisa TEHAMA wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (MUHAS) Bw. Awadh Mnyika baada ya kuridhika na mafunzo aliyopewa ya kumwezesha kuhuisha tovuti yao.

Kauli ya Mnyika ilitolewa wakati wa kufunga mafunzo ya kupandisha taarifa kwenye tovuti ya MUHAS yaliyofanyika katika ofisi za Wakala ya Serikali Mtandao (eGA) Februari 23 hadi 25, 2016. Mafunzo hayo yalihusisha maofisa TEHAMA wanne  kutoka chuo hicho yaliyolenga kuwajengea uwezo wa kuweza kupandisha na kuhuisha taarifa mbalimbali za chuo chao kwa manufaa ya wananchi kwa jumla.

Mratibu wa mafunzo hayo, Ofisa TEHAMA Mkuu, Bi. Fatma Mgembe amewataka maofisa TEHAMA kuhakikisha wanatatua matatizo ya kiufundi pale yanapojitokeza huku Ofisa habari/Uhusiano/Mawasiliano akipandisha taarifa kwenye tovuti hiyo. Aidha, amewataka maofisa hao kuwasiliana na Wakala kupitia dawati la huduma kwa mteja kwa anwani ya egov.helpdesk@ega.go.tz kwa tatizo lolote la kiufundi ili waweze kupata msaada wa haraka.

Ofisa TEHAMA wa MUHAS Bw. Awadh Mnyika  alisema, tovuti yao, inayopatikana kwa anwani ya www.muhas.ac.tz itakuwa na tija kwa chuo hicho kwa kuwa wanafunzi wa ndani na nje ya nchi watapata taarifa mbalimbali za chuo na hivyo kujiunga kwa wingi.

Vile vile, Bi. Rebecca Chaula ambaye pia ni Ofisa TEHAMA wa chuo hicho alisema “Hivi sasa taarifa katika tovuti yetu zimekaa katika mpangilio mzuri na wenye kuvutia kwa msomaji . Hii ni kwa sababu ya usanifu mzuri na bora”.

Wakala imekuwa ikisanifu na kutengeneza tovuti mbalimbali za Serikali ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa kwa umma. Pia imekuwa ikiendesha mafunzo ili kuwajengea uwezo na ujuzi maafisa mbalimbali katika kuandaa, kuhuisha na kupandisha taarifa mbalimbali za taasisi kwa ajili ya tovuti zao.