emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Mahakama yawanoa Maofisa TEHAMA wake


Mahakama yawanoa Maofisa TEHAMA wake


Maofisa TEHAMA wa mahakama wametakiwa kutumia ujuzi watakaoupata kutatua matatizo mbalimbali kwa ufanisi katika kazi za Mahakama na kushirikiana na watumishi wenzao ili kuongeza ubunifu wa kuboresha huduma za mahakama.

Hayo yalisemwa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Bw. Hussen Kattanga wakati wa uzinduzi wa Mafunzo kwa Maofisa hao Januari 16, 2017 katika Ukumbi wa Mafunzo wa Shule ya Sheria jijini Dar es Salaam.

“Ni matumaini yangu mtakapomaliza mafunzo haya na elimu mtakayoipata hapa kila mmoja ataitumia vizuri hasa katika kuongeza ubunifu na kutatua changamoto mbalimbali za masuala ya TEHAMA” alisema Bw. Kattanga.

Vilevile Bw. Kattanga aliwausia watumishi hao kuwa ujuzi watakaopata katika mafunzo hayo usiishie hapo bali watakapofika kwenye maeneo yao ya kazi wawafundishe na watumishi wengine ili na wao waweze kuwa na ujuzi zaidi.

Akitoa Mada katika Mafunzo hayo, Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali Mtandao, Dkt. Jabir Bakari amesema kuwa lengo kuu la Wakala hii ni kuwa na dirisha moja linalotoa huduma za serikali Mtandao kwa wananchi zenye lengo la kuleta ubora, kupunguza gharama na kusaidia ukusanyaji wa mapato ya Serikali kupitia njia za Kielektroni.

Aidha Dkt Bakari alisema kupitia Wakala hii Mifumo mbalimbali ya Kielektroni imeweza kutengenezwa na kutumiwa na taasisi za Serikali na kusaidia uboreshaji wa utoaji wa huduma za Serikali kwa umma.

Mafunzo hayo yatakayofanyika kwa muda wa wiki moja yamewahusisha takribani maofisa TEHAMA 25 kutoka katika kanda zote za Mahakama Tanzania.