Watumishi wa wakala ya Serikali Mtandao wameaswa kupima afya zao mara kwa mara ili kuhakisha afya haziteteleshwi na magonjwa ambukizi na hata yale yasiyoambukiza.
Hayo yamesemwa na Mtendaji Mkuu wa Wakala Dkt. Jabiri Bakari wakati akifungua semina ya afya ambayo ilitanguliwa na mafunzo elekezi kisha upimaji wa afya iliyofanyika katika ukumbi wa wakala Desemba 3, 2015.
Dkt. Bakari amesema Serikali imekuwa ikifanya juhudi mbalimbali katika kupambana na VVU, UKIMWI na Magonjwa yasiyoambukiza (MSY) mahala pa kazi. Katika juhudi hizo miongozo pamoja na nyaraka mbalimbali zimekuwa zikitolewa ili kupambana na majanga haya na kuweza kuboresha utendaji kazi Serikalini
“Tumeunda kamati ya kudhibiti Ukimwi na magonjwa yasiyoaambukiza ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la serikali pia kama sehemu ya jitihada za kupambana na magonjwa ambayo yanaweza kuharibu nguvu kazi ya Wakala. Kama hali ya afya si nzuri vivyo hivyo itakuwa vigumu kufikia malengo wakala iliyojiwekea kwani nguvu kazi iliyopo inakuwa sio mwafaka” Alisema Dkt. Bakari
Dkt. Bakari aliongeza kuwa lengo mahususi katika zoezi hilo ni kuhakikisha kuwa kila mtumishi wa wakala anafahamu hali ya afya yake kwa kuwa magonjwa haya yanachangia kupotea kwa kiasi kikubwa cha nguvu kazi tuliyonayo si kwa wakala pekee bali hata kwa taifa zima, hivyo kuathiri utendaji kazi wa Wakala na katika utumishi wa umma kwa jumla.
Vilevile, Mkurugenzi wa Huduma na Uwezeshaji Bw. Ibrahim Mahumi amesisitiza kuwa, ni muhimu kwa kila mtumishi kuwa na uthubutu na kujiwekea utaratibu wa kupima afya mara kwa mara ili kuweza kujitambua na hivyo kuishi kwa kuzingatia matakwa ya kanuni za afya.
Alieleza kuwa,katika semina hii hakutakuwa na kipimo cha ugonjwa wa ukimwi lakini aliwasihi watumishi kwenda kupima na kutambua hali ya afya zao kwa kuzingatia Sheria Namba 2 ya Kuzuia na Kupambana na Ukimwi ya 2008 ambayo inampa fursa mtu yeyote aishiye Tanzania kwa hiari yake kupima afya yake kwa kupima VVU bila kulazimishwa.
“Shughuli ya leo ya kushauriwa na kupima afya ni sehemu ya hatua za utekelezaji wa maazimio ya kamati ya kudhibiti UKIMWI na magonjwa yasiyoaambukiza na ni moja ya agenda za kudumu katika mpango kazi wa Wakala. Pia, sisi kama Wakala tumeanzisha klabu ya michezo ili kuhakikisha afya za watumishi wetu zinakuwa imara wakati wote”alisema Bw. Mahumi
Alisisitiza pia kuwa, madhumuni ya Waraka wa watumishi wa umma Na.2 wa mwaka 2006 kuhusu huduma kwa watumishi wa umma wanaoishi na virusi vya ukimwi na wenye ukimwi ni kuweka utaratibu rasmi wa namna ya kutoa huduma kwa watumishi wanaoishi na virusi vya ukimwi na wenye ukimwi ili wawe na afya njema ya kuwawezesha kutumia ujuzi na taaluma walizozipata kwa gharama kubwa kwa faida yao, familia zao, pamoja na taifa zima kwa kutoa huduma bora.
“Usifurahi kuona mwenzako ni mgonjwa wala usimwambukize mwenzako kwa makusudi kwa kuwa sheria inatambukua kuwa hilo ni kosa na kuna adhabu yake”alisema Mahumi.
Aliongeza kuwa, kwa mujibu wa Sheria Namba 2 ya Kuzuia na Kupambana na Ukimwi ya 2008, kifungu cha 47 kinatoa adhabu kwa watu wote wenye nia mbaya ya kuambukiza wengine ugonjwa wa UKIMWI kwa njia yoyote ile. Kifungu hicho kinasema kuwa, mtu yeyote ambaye atamwambukiza mtu mwingine VVU kwa makusudi, atakuwa amefanya kosa na itakapothibitika ataadhibiwa kifungo kisichopungua miaka mitano na kisichozidi miaka kumi.
Vilevile, katika ulimwengu wa imani na hata katika vitabu vya dini Mungu anakataza na kulaani kitendo hicho kwa mfano katika Uislamu unasema anayeua nafsi moja ni sawa na kuua nafsi zote. Pia ipo Hadithi ya Mtume (SwallaAllahu Alayhi Wasalam) inayosema “Aliye na maradhi asimuambukize asiyekuwa nayo.” alisisitiza
Aidha, aliwataka watumishi wa Wakala kujitokeza kupima na kujua hali ya afya zao ili wote ambao bado hawajaambukizwa waendelee kuwa salama na watabainika kwa wakati wowote kuwa wana maambukizi ya virusi vya ukimwi watapatiwa huduma zinazostahili na kuzuia maambukizi mapya.
Naye Dkt. Godwin Ndeki kutoka Taasisi ya Teknolojia Dar es salaam (DIT) aliipongeza Wakala kwa kuajiri vijana walio na umri kati ya 30-39. Pia, aliwasihi watumishi hao kuwa wazi kwa mwajiri wao endapo wana tatizo lolote la kiafya ili waweze kupunguziwa majukumu yanayoweza kuhatarisha uhai wao.
“Kufahamu afya yako mapema kuna manufaa kwa kuwa utagundua maradhi yakiwa katika hatua za awali kabla ya hayajawa sugu, hivyo kupata muda wa kuyatibu mapema” alisema Ndeki.
Aidha, alizungumzia suala la msongo wa mawazo ambao huweza kusababishwa na mazingira, shughuli za kila siku pamoja na uhusiano wa aina zote. Alisema ni vizuri kuweza kuukabili msongo ili kuwa na afya njema na hivyo kuongeza ufanisi na utendaji kazi mahali pa kazi.
“Unaweza kudhibiti msongo kwa kufanya mazoezi ya viungo, kubadilisha mtazamo wako juu ya jambo unalofikiri, kupata ushauri wa kitaalam pamoja na kuzungumza na watu wengine wanaokuzunguka”, alisema Dkt. Ndeki
Naye., mmoja wa watumishi wa Wakala Bw. Othman Omary amesema amefahamu kuwa magonjwa yasiyoambukiza kama vile kisukari, saratani na shinikizo la damu ni hatari zaidi kwa kuwa ndiyo yanayoongoza kuondoa uhai wa binaadam.
“Nimefurahi sana kupata mafunzo ya afya kwani nimejua umuhimu wa kupima na wakati muafaka wa kupima”, alisema Bw. Omary.
Naye Bi.Diana Mlokozi amesema amejifunza jinsi ya kumudu msongo wa mawazo pamoja na kuishi kwa kufuata kanuni za afya kwa kula vizuri na kufanya mazoezi ili kuwa na uzito unotakiwa ambao si chini ya BMI 20 na si zaidi ya 24.9.