emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Maofisa Wapewa mafunzo


Maofisa Wapewa mafunzo


Maofisa Habari kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Halmashauri ya Jiji la Mbeya wametakiwa kuandaa na kupandisha taarifa katika tovuti zao mara kwa mara ili wananchi waweze kupata taarifa mpya na zinazoenda na wakati.

Hayo yamesemwa na Meneja Mawasiliano wa Wakala ya Serikali Mtandao Bi. Suzan Mshakangoto alipofungua mafunzo kwa taasisi hizo yaliyofanyika katika ofisi za Wakala kwa siku nne kuanzia Februari 16 hadi 19, 2016.

“Wakala inatoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kuziendesha tovuti na kuhakikisha kuwa mnaweka taarifa zenye lengo la kusaidia umma kujua huduma na shughuli zinazofanywa na taasisi za umma. Hivyo ni jukumu la kila mshiriki kuhakikisha anaelewa dhana ya mafunzo haya ikiwa ni pamoja na kuhakiki taarifa hizo kabla ya kuzipandisha kwenye tovuti”. alisema Bi. Mshakangoto

Ofisa habari wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya Bi.Jaqueline Msuya amesema tovuti yao itakayopatikana kupitia anwani ya www.mbeyacc.go.tz itasaidia wananchi kujua shughuli mbalimbali zinazofanywa na taasisi hiyo zikiwemo huduma wanazozitoa kwa wananchi wa jiji hilo na dunia kwa jumla.

“Tumeamua kutengeneza tovuti ili kurahisisha mawasiliano kati ya Halmashauri na wananchi, vilevile kupitia tovuti hii wananchi wataweza kutuandikia maswali mbalimbali yatakayotolewa ufafanuzi ili kuwa na uwelewa wa pamoja,”alisema Bi. Msuya

Naye, Bw. John Kiluwa ambaye pia ni Ofisa habari wa Jiji hilo alisema tovuti hiyo itasaidia katika kuitangaza halmashauri yao. Aidha, wananchi wataweza kupata matangazo mbalimbali yakiwemo ya vikao vya wazi vya madiwani ambapo wanaruhusiwa kushiriki.

“Kupitia tovuti hii wananchi wa jiji la Mbeya watafahamu shule mbalimbali zinazosimamiwa na Halmashauri yetu, matokeo ya shule hizo na ubora wake”, alisisitiza Bw. Kiluwa.

Vilevile, Ofisa Habari kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bi. Eliafile Solla amesema kupitia tovuti hiyo itakayopatikana kupitia anwani ya www.ardhi.go.tz wananchi watafahamu huduma mbalimbali zinazotolewa na Wizara na namna ya kuzipata huduma hizo.

“Tovuti hii itamsaidia mwananchi kupata huduma bila kufika ofisini kama vile suala la ulipaji kodi ya ardhi, upo mfumo maalum wa kulipia kodi hiyo unaoitwa Mfumo wa Kadirio la Kodi ya Ardhi ambao umeunganishwa kwenye tovuti hii. Kupitia mfumo huu, mwananchi anaweza kukamilisha malipo yake yatakayopokelewa kupitia mfumo huo”, alifafanua Bi. Solla.

Naye Ofisa TEHAMA wa Wizara hiyo, Bi. Yenala Mwangwale amesema mwananchi atakuwa akituma maswali yake na kupata mrejesho ndani ya siku tatu na hivyo kusaidia katika kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali na kupunguza kero kwa wananchi.