emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Makabidhiano ya Mfumo wa Taarifa za Mashauri


Makabidhiano ya Mfumo wa Taarifa za Mashauri


Mkurugenzi wa Usimamizi wa Huduma za TEHAMA wa Wakala ya Serikali Mtandao (eGA) Injinia Benedict Ndomba amesema Wakala imeamua kutumia utajiri wa utaalamu wake wa TEHAMA kutengeneza mifumo mbalimbali inayosaidia taasisi za umma kutekeleza majukumu yake kwa haraka, ubora na kwa ufanisi zaidi.

Injinia Ndomba amesema hayo leo tarehe 7 Juni, 2019 katika Ofisi za Wakala ya Serikali Mtandao Dar es Salaam alipokuwa akiongea na Waandishi wa Habari wakati wa kukabidhi Mfumo wa Taarifa za Usimamizi wa Mashauri kwaWakili Mkuu wa Serikali Dkt. Clement Julius Mashamba.

“Serikali hii ya awamu ya tano ina hazina kubwa ya wataalamu wa TEHAMA, kielelezo kimojawapo ni kuwa mfumo huu umebuniwa, umesanifiwa na kutengenezwa watumishi wa umma na tumekubaliana na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kuwa mfumo huu ni mkubwa, utekelezwe kwa awamu mbalimbali ili kukidhi mahitaji ya wadau wote katika tasnia hii”.

Ameongeza kuwa katika awamu ya kwanza imetengenezwa moduli itakayosaidia Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kutekeleza majukumu na shughuli mbalimbali za ndani hasa katika masuala yanayohusiana na usimamizi wa majalada ya mashauri”.

Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa mfumo huo, Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Clement Julius Mashamba ameipongeza Wakala kwa kutengeneza mfumo kwa wakati na kuzingatia mahitaji yaliyoainishwa na Ofisi yake.

“Ofisi yangu itaendelea kushirikiana na Wakala ya Serikali Mtandao kuhakikisha awamu zote za utengenezwaji wa mfumo huu zinatekelezwa kwa wakati na kwa ubora unaostahili. Aidha, ni dhahiri kuwa ofisi yangu inatambua mchango mkubwa na manufaa ya TEHAMA katika kuharakisha utoaji haki na pia inasogeza huduma karibu zaidi na wadau” Amesema Dkt. Mashamba.

Dkt. Mashamba amesema kuwa mfumo unaiwezesha Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kufanya shughuli muhimu zikiwemo: usimamizi wa majalada ya mashauri, usajili wa mashauri, upangaji wa mashauri yanayoshughulikiwa, ufuatiliaji wa maendeleo ya mashauri, usimamizi wa ratiba ya mashauri, utoaji taarifa, uhakiki wa mwenendo wa mashauri na uhamishaji wa taarifa na takwimu pale inapobidi.

Ameongeza kuwa, mfumo huu utasaidia kuboresha usimamizi wa mashauri ikiwa ni pamoja na kudhibiti ubora wa huduma zinazotolewa na ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, pia mfumo utasaidia katika kuongeza kasi ya utendaji wa shughuli za ofisi, hivyo kusaidia katika upatikanaji wa haki kwa wakati.

Faida za kutumia mfumo huu ni kuwa unaweza kutumiwa na idara mbalimbali za serikali, unapatikana mahali pamoja, umegawanywa katika sehemu ndogondogo kwa ajili ya matumizi na unatoa ripoti ya uchambuzi wa taarifa na takwimu, lakini pamoja na hayo ni rahisi kwa mtumiaji.

Faida nyingine ya mfumo huu ni kuwa unaruhusu utanzuaji wa mashauri ya kughushi na kutoa taarifa za ukiukaji wa sheria, kanuni na taratibu. Pia unaisaidia kupanua wigo wa uelewa kwa wananchi na kujibu ipasavyo hoja mbalimbali za bunge, vyombo vya habari na wadau wengine muhimu kwa taarifa sahihi na kwa wakati.

Aidha, Dkt. Mashamba amefafanua kuwa mfumo huu utaunganishwa na mifumo mingine ya wadau nje ya ofisi ili kurahisisha ubadilishanaji wa taarifa.