Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu mjini DODOMA (CDA) imesema itatumia Mfumo wa Huduma za Serikali kupitia simu ya Mkononi ili kuwafikia wananchi kwa haraka na kurahisisha utoaji wa taarifa na huduma kwa wateja wake.
Hayo yamebainishwa na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mazingira wa CDA Bi. Marry Boba katika kikao cha pamoja kati ya Wakala na Menejimenti ya Mamlaka hiyo kilichofanyika mjini DODOMA Juni 26, 2015.
Wajumbe wa Menejimenti hiyo walitaka kufahamu uhusiano wa Mfumo wa Malipo ya Mishahara ya Watumishi (payroll) na Mfumo wa Barua Pepe Serikalini (GMS) ambapo Mkurugenzi wa Usimamizi wa Huduma za TEHAMA wa Wakala ya Serikali Mtandao (eGA), Bw. Benedict Ndomba alisema ni lazima uwe mtumishi halali wa Serikali ndipo utatumia mfumo wa GMS na barua pepe zote zimeunganishwa kwenye mfumo huo.
“Namba ya utambulisho ya mtumishi (cheque number) ya mtumishi imeunganishwa kwenye mfumo wa GMS na kama mtumishi akipata tatizo lolote kwenye orodha ya wapokea mshahara (payroll) yake kwa kubadilisha taarifa zake za akaunti anayotumia au kwa sababu nyingine, hataweza kutumia mfumo huo”, alisema Bw. Ndomba
Naye Meneja wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano wa Wakala, Bi. Suzan Mshakangoto aliishauri Mamlaka hiyo kuweka taarifa zake katika Tovuti Kuu ya Serikali na kupata nafasi ya kujibu maswali ya wananchi katika tovuti rasmi ya wananchi.
Wakala ya Serikali Mtandao inatembelea taasisi za Serikali kwa lengo la kujitangaza na kunadi huduma mbalimbali zinazotolewa na Wakala za kuwezesha taasisi hizo kutoa huduma bora kwa wananchi.