Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali Mtandao (eGA) Dkt. Jabiri Bakari amewataka wakandarasi wa mradi wa Mtandao wa Serikali (GovNet) kuhakikisha huduma hiyo inapatikana kwa takriban taasisi 20 za Umma zilizoonesha utayari wa kuanza kutumia Mfumo wa Mtandao wa Serikali kuanzia Mei 1, 2015.
Dkt. Bakari amesema hayo wakati wa kikao cha wadau wa “GovNet” kutoka Wizara, Idara zinazojitegemea na Wakala za Serikali kilichofanyika Aprili 27, 2015 katika hoteli ya Giraffe Ocean View, Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza kwenye kikao hicho, Dkt. Bakari amesema mradi huo una sehemu tatu “GovNet Phase I,II na III” ambazo zinahusisha mambo mbalimbali kama vile uwekaji wa “Bandwidth” ya Serikali, “Network”, kurekebisha na kuweka “LANs”,kwa Wizara, Idara na Wakala za Serikali, ufungaji wa “IP PBX” na “IP Phones”.
“Taasisi za Serikali zipatazo 72 zimeshaunganishwa na Halmashauri 77 zitaunganishwa kwenye mradi huo. Wizara ishirini na sita (26) zitaunganishwa kwenye Mtandao wa Serikali wa ndani (LANs), na takriban Wizara, Idara na Wakala za Serikali 60 nazo zitaunganishwa mwishoni mwa Aprili, 2015”, alisema Dkt. Bakari.
Ameongeza kuwa mradi huo utazisaidia taasisi za Umma kuwa na mawasiliano yaliyo salama, utaipunguzia Serikali gharama za simu na kuongeza kasi ya “bandwidth” katika kutekeleza majukumu yao ya kuwahudumia wananchi.
Vilevile Dkt. Bakari amesema mradi wa Govnet ukikamilika, tovuti zote zenye taarifa zisizofaa pamoja na mitandao ya kijamii havitapatikana kwenye kompyuta ya mtumishi yeyote wakati wa saa za kazi ili kutoa nafasi kwa watumishi kutekeleza wajibu wao kwa ufanisi.
Naye Meneja wa Idara ya Mtandao wa Serikali Bw. Ricco Boma amesema,lengo la kukutana na wadau hao ni kuweza kutoa taarifa kuhusu kile kilichofanyika na kinachoendelea kufanyika katika mradi huo, kuwapa taarifa kuhusu miradi mingine inayokuja , kuwawezesha wadau kukutana na wakandarasi wanaotekeleza mradi huo na pia kuendeleza ushirikiano mzuri kati ya Wakala na taasisi nyingine za Umma.
Akizungumzia changamoto zilizopatikana wakati wakitekeleza mradi huo kwa awamu ya kwanza na pili, Bw. Boma amesema zipo baadhi ya taasisi za Serikali ambazo muda wa kazi ukiisha hufunga ofisi bila kujali umuhimu wa kazi inayofanywa na wakandarasi, vilevile baadhi ya watumishi wanaohudhuria mafunzo kutokuwa tayari kuwasilisha maarifa au ujuzi walioupata kwa maafisa wengine.
“Baadi ya taasisi za Serikali hufunga ofisi mara baada ya muda wa kazi kumalizika hali inayofanya utekeliezaji wa mradi wa GovNet kuwa mgumu”, alisema Bw. Boma.
Mshiriki kutoka Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Bw. Victor Rweyemamu amesema mradi wa GovNet ni muhimu kwa kuwa utarahisisha utekelezaji wa shughuli za Serikali na kuwahudumia wananchi kwa wakati.
Naye Afisa TEHAMA kutoka Tume ya Mipango, Bi. Catherine Mlimbila amesema Mtandao wa Serikali ni muhimu kwa kuwa utarahisisha mawasiliano kwa taasisi za Umma pamoja na kuleta usalama wa taarifa za Serikali.
Kikao hicho cha wadau kiliandaliwa na Wakala ambapo mada kuhusu utekelezaji wa Serikali Mtandao iliwasilishwa pamoja na ripoti ya Utekelezaji wa mradi wa Mtandao wa Serikali (GovNet).