emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

WADAU 1000 WA SERIKALI MTANDAO KUKUTANA FEBRUARI JIJINI ARUSHA


WADAU 1000 WA SERIKALI MTANDAO KUKUTANA FEBRUARI JIJINI ARUSHA


Takriban wadau 1000 wa serikali mtandao wanatarajiwa kukutana kwa siku tatu, kuanzia Februari 11 hadi 13, 2025 jijini Arusha, ili kujadiliana kuhusu hali ya utekelezaji wa Serikali Mtandao nchini, kuainisha changamoto, sambamba na kuweka mikakati ya pamoja ya kukabiliana na changamoto hizo.

Wadau hao kutoka katika taasisi na mashirika mbalimbali ya umma, wanatarajiwa kukutana katika Mkutano (5) wa mwaka wa Serikali Mtandao, utakaofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC).

Akizungumza kuhusu mkutano huo, Meneja Mawasiliano wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Bi. Subira Kaswaga amesema, mkutano huo utazinduliwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuoneshwa mubashara katika vyombo mbalimbali vha habari na mitandao ya kijamii.

Ameongeza kuwa, mkutano huo utawakutanisha viongozi na watumishi mbalimbali wa sekta ya umma wakiwemo Makatibu Wakuu, Maafisa Masuuli, Wakurugenzi na Wakuu wa Idara na vitengo vya TEHAMA, Maafisa TEHAMA pamoja na Maafisa wa kada nyingine.

“Lengo la mkutano huo ni kuwakutanisha wadau wa Serikali Mtandao kutoka katika taasisi na mashirika ya umma, ili waweze kujadili kwa pamoja jitihada mbalimbali za utekelezaji wa Serikali Mtandao, na kuweka mikakati itakayosaidia kukuza jitihada hizo”, amefafanua Bi. Subira.

Ameongeza kuwa, mkutano huo unatarajiwa kuongeza uelewa kwa washiriki kuhusu serikali mtandao, teknolojia mpya zinazoibukia sambamba na namna zinavyoweza kutumika katika kuimarisha utendaji kazi serikalini na kurahisisha utoaji wa huduma bora kwa umma.

“Mkutano huo utaongozwa na kauli mbiu isemayo “Utekelezaji wa Jitihada za Serikali Mtandao na Ubunifu kwa utoaji wa huduma bora kwa umma ikiwa na lengo la kuchochea ubunifu na utekelezaji wa Jitihada za Serikali Mtandao kwa Taasisi za Umma, ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi na utoaji wa huduma bora kwa umma”, amesema Bi. Subira.

Amefafanua kuwa, katika mkutano huo, e-GA itawasilisha taarifa ya utekelezaji wa maazimio 12 yaliyofikiwa katika Mkutano wa nne (4) wa Serikali Mtandao uliofanyika Februari 2024.

“Katika mkutano uliopita, wadau waliweka maazimio 12 yaliyolenga kuboresha utendaji kazi na utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao, hivyo mwaka huu tutawasilisha taarifa ya utekelezaji wa maazimio hayo kwa washiriki wote” ameeleza Bi. Subira.

Aidha, Bi.Subira ametoa rai kwa wadau wote wa Serikali Mtandao kutoka sekta ya umma kujitokeza kwa wingi na kushiriki kikamilifu katika mkutano huo, kwa kujisajili kupitia mfumo wa mafunzo na semina (TSMS) unaopatikana kwa kikoa cha www.tsms.ega.go.tz.