Ufanisi wa Serikali Mtandao hutegemea usimamizi mzuri wa rasilimali, ushirikiano wa wadau, na utekelezaji wa mikakati madhubuti ili kuiwezesha Serikali kutoa huduma bora, kupunguza urasimu, na kuongeza uwazi, na hatimaye kuboresha maisha ya wananchi.
Katika kuhakikisha usimamizi thabiti wa Serikali Mtandao nchini, Kifungu cha 15 cha Sheria ya Serikali Mtandao Namba 10 Sura ya 273 ya Mwaka 2019 (Sheria), kinaelekeza juu ya uanzishwaji wa muundo na michakato ya Serikali-mtandao katika utumishi wa umma, ambapo kamati mbalimbali za Uongozi za Serikali Mtandao katika taasisi za umma zimeanzishwa.
Kamati hizo ni Kamati ya Kitaifa ya Uongozi ya Serikali-mtandao, Kamati ya Ufundi ya Serikali-mtandao na Kamati ya Kitaasisi ya Uongozi ya Serikali-mtandao.
Lengo kuu la kuanzisha kamati hizi, ni kutoa miongozo katika kusimamia na kudhibiti utekelezaji wa matumizi sahihi ya TEHAMA katika taasisi zote za umma zikiwemo Wizara, Halmashauri, Mashirika ya Umma na Idara za Serikali zinazojitegemea.
Kifungu cha 16 (1) cha Sheria kinaanzisha Kamati ya Kitaifa ya Uongozi ya Serikali Mtandao (National e-Government Steering Committee), kwa ajili ya kusimamia masuala ya kitaifa ya Serikali Mtandao.
Pia kifungu cha 16(2) cha Sheria, kinatoa muundo wa kamati hiyo ambayo itaundwa na Katibu Mkuu Kiongozi ambaye ndiye atakua Mwenyekiti wa kamati na Katibu Mkuu wa Wizara yenye dhamana na kusimamia Serikali Mtandao ndiye atakua Katibu.
Wajumbe wengine wa kamati hii ni Katibu Mkuu wa Wizara yenye dhamana na TEHAMA (Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari), Katibu Mkuu wa Wizara yenye dhamana na fedha (Wizara ya Fedha), Katibu Mkuu wa Wizara yenye dhamana na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA).
Aidha, Wizara yenye dhamana na Serikali Mtandao, itatumika kama sekretarieti ya Kamati ya Kitaifa ya Uongozi ya Serikali Mtandao.
Meneja wa Kitengo cha Huduma za Sheria e-GA, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Raphael Rutaihwa, amebainisha kwamba kamati hii imekasimiwa majukumu matano (5) makubwa ikiwemo, kutoa miongozo ya kimkakati na kisera inayohitajika kuendesha mabadiliko ya utoaji na utawala wa huduma za umma katika zama za kidijiti.
Ameongeza kuwa, kamati hii pia imepewa jukumu la kuidhinisha sera mtambuka za TEHAMA, mikakati, mpango mkuu na miongozo katika Serikali pamoja na kushauri juu ya miradi na mipango muhimu ya TEHAMA, ili kuhakikisha matumizi shirikishi na ya gharama nafuu ya TEHAMA katika Serikali.
“Vilevile, kamati hii imepewa jukumu la kumshauri Waziri mwenye dhamana juu ya masuala yote yanayohusu Serikali Mtandao, na kutekeleza majukumu mengine kama ambavyo Waziri anaweza kuelekeza”, amefafanua SACP Rutahiwa.
Aidha, Kifungu cha 17(1) cha Sheria kimemtaka Waziri mwenye dhamana ya Serikali Mtandao, kuunda Kamati ya Ufundi ya Serikali Mtandao (e-Government Technical Committee), kwa ajili ya kutoa mwongozo wa kiufundi kwa taasisi za umma juu ya utekelezaji wa mipango ya TEHAMA.
Kwa mujibu wa kifungu cha 17(2) cha Sheria, Wajumbe wa Kamati hii watateuliwa kutoka miongoni mwa Wakuu wa Idara na Vitengo vya TEHAMA katika Wizara, na Wakurugenzi wa Ufundi wa TEHAMA wa taasisi za umma ambazo zimetajwa kisheria.
Mwenyekiti wa Kamati hii atateuliwa na Waziri na Katibu atateuliwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), kama ambavyo kifungu cha 17(3) cha Sheria kinaelekeza.
Aidha, Kamati hii ya Ufundi chini ya kifungu cha 17(4) cha Sheria ina jukumu la kupitia na kupendekeza juu ya sera ya Serikali Mtandao, kwa ajili ya matumizi ya taasisi zote za umma.
Pamoja na majukumu mengine ya msingi kama vile kuidhinisha viwango vya Serikali Mtandao, kupitia na kupendekeza juu ya miradi na mipango muhimu ya kitaifa ya Serikali Mtandao, pamoja na kuishauri Kamati ya Kitaifa ya Uongozi ya Serikali-mtandao juu ya masuala yote yanayohusiana na Serikali-mtandao.
Aidha, kamati ya Ufundi ya Serikali Mtandao, katika utekelezaji wa majukumu yake chini ya Sheria hii, itawajibika na kuripoti kwa Kamati ya Kitaifa ya Uongozi ya Serikali-mtandao, kwa kuaandaa taarifa ya shughuli zake kila robo mwaka na kuiwasilisha kwa Kamati ya Uongozi ya Serikali Mtandao, kama ambavyo kifungu cha 17(5) na (6) cha sheria ya Serikali Mtandao kimeelekeza.
Kamati hii pia, kwa ajili ya utendaji bora wa majukumu yake chini ya kifungu kidogo cha (4) imepewa nguvu ya kuunda kamati ndogo kwa idadi itakayofaa, ili kutekeleza majukumu ya kiufundi kama inavyoweza kuamua, lengo ni kuhakikisha kamati hii inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.
Kamati nyingine ni ile inayopaswa kuundwa katika ngazi ya taasisi, Kifungu cha 18 (1) cha Sheria kinamtaka kila Afisa Masuuli wa taasisi ya umma kuunda Kamati ya Kitaasisi ya Uongozi ya TEHAMA (Institutional ICT Steering Committee) ambayo itasimamia utekelezaji wa muongozo wa TEHAMA katika taasisi husika.
Lengo ni kuhakikisha miradi na mifumo yote ya TEHAMA inazingatia Sheria ya Serikali Mtandao na kuleta tija kwa taasisi husika kulingana na thamani halisi ya uwekezaji iliyowekwa.
Sambamba na hilo, Kifungu cha 18(2) cha Sheria, kinaelekeza uundaji wa Kamati ya Kitaasisi ya Uongozi ya TEHAMA ambayo itaundwa na wajumbe wasiopungua sita (6) na wasiozidi saba (7) kama ifuatavyo; Afisa Masuuli wa taasisi husika atakuwa Mwenyekiti na Mkuu wa Idara/Kitengo cha TEHAMA ambaye atakuwa katibu wa Kamati.
Wajumbe wengine ni Mkuu wa Mipango; Mkuu wa Ununuzi; Mkaguzi Mkuu wa Ndani; Mhasibu Mkuu; na angalau Mkuu mmoja wa Kitengo au Idara inayohusika na shughuli kuu ya biashara inayozalishwa katika taasisi (head of key business unit).
Kamati ya Kitaasisi ya Uongozi ya TEHAMA itatekeleza majukumu makuu saba (7) kama yalivyoainishwa chini ya kifungu cha 18(3) cha Sheria ikiwemo; kukagua na kupitisha sera na mikakati ya TEHAMA ya taasisi; kukagua na kutoa ushauri juu ya uwekezaji wa TEHAMA na vipaumbele vyake.
Majukumu mengine ni kuhakikisha ufuatiliaji na tathmini endelevu ya miradi ya TEHAMA ya kitaasisi; kukagua na kupitisha mipango ya maafa ya kitaasisi na hakikisha utekelezaji wake unafanikiwa.
Aidha, kifungu cha 18(7) cha Sheria kimeelekeza kamati hii kuwajibika kuandaa na kuwasilisha ripoti ya robo mwaka kwa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), ikieleza maendeleo ya jitahada za Serikali Mtandao katika taasisi husika; na kutekeleza majukumu mengine kama inavyoweza kuelekezwa na Afisa masuuli au Mamlaka.
Hadi sasa uwepo wa Kamati ya Uongozi za Serikali Mtandao katika Taasisi za Umma zikiwemo halmashauri, zimeongeza ufanisi katika matumizi ya serikali mtandao nchini na kuhakikisha miongozo na viwango vya Serikali Mtandao vinatekelezwa ipasavyo.
Meneja wa Usimamizi wa Udhibiti na Viwango vya Serikali Mtandao wa e-GA Bi. Sultana Seiff, amebainisha kwamba kamati hizo zimekuwa kiungo muhimu katika ukuzaji wa jitihada za Serikali Mtandao katika taasisi za umma na kurahisisha huduma za serikali kwa wananchi.
“Kamati hizi zina mchango mkubwa katika kukuza na kuimarisha matumizi ya TEHAMA ndani ya taasisi, ikiwemo utekelezaji wa miradi mbalimbali ya TEHAMA ambayo inachangia katika kuongeza ufanisi wa utendaji kazi ndani ya taasisi na kuboresha utoaji wa huduma bora kwa wananchi,” amesisitiza Bi. Sultana.
Ameongeza kuwa, kamati hizi pia zimekuwa kiungo muhimu katika utekelezaji wa Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao katika matumizi ya TEHAMA ndani ya taasisi husika.
Kwa upande wake SACP Rutaihwa ametoa rai kwa taasisi zote za umma zikiwemo halmashauri kuanzisha kamati za Uongozi wa TEHAMA ndani ya Taasisi zao. ili kukidhi takwa la kifungu cha 18 cha Sheria ya Serikali Mtandao.
Usimamizi na uendeshaji wa serikali mtandao unatoa fursa kubwa ya kuboresha utendaji wa serikali, kuongeza uwazi, na kuboresha huduma kwa wananchi. Kwa kutumia TEHAMA, serikali ina uwezo wa kufikia wananchi wengi kwa urahisi zaidi, kutoa huduma kwa ufanisi, na kupunguza urasimu.
Ili kufanikisha malengo haya, ni muhimu viongozi wa taasisi za umma kuhakikisha wanaunda kamati za uongozi wa TEHAMA katika taasisi zao sambamba na kamati zote tatu kuhakikisha zinatekeleza majukumu yake kwa ufanisi na weledi kama yalivyoainishwa katika sheria.