Napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kuuona Mwaka Mpya wa 2025, kwa niaba ya Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), napenda kuwatakia nyote Heri ya Mwaka Mpya 2025.
Mamlaka ya Serikali Mtandao, inapenda kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuiwezesha e-GA kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Katika mwaka uliopita (2024), e-GA imeweza kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kuratibu, kusimamia na kukuza jitihada za Serikali Mtandao pamoja na kuhimiza utekelezaji wa Sera, Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao kwa taasisi za umma.
Utekelezaji wa majukumu haya, unatokana na mchango mkubwa wa Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Ofisi ya Rais, kwa kutenga bajeti na kuisimamia vema e-GA, ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.
Pamoja na mafanikio haya, Mwaka huu mpya wa 2025 unaleta fursa mpya, changamoto, na matumaini mapya kwa Mamlaka, kuongeza jitihada na kuboresha mikakati ya kuziwesha Taasisi za Umma kutumia TEHAMA katika utendaji kazi wake, ili kuongeza ufanisi pamoja na kuboresha utoaji wa huduma bora kwa umma.
Ili tufikie malengo ya kuwa na Serikali Mtandao imara na yenye tija, jitihada za pamoja zinahitajika kwa wadau wote wa Serikali Mtandao, kwa kuhakikisha wanazingatia Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao katika ujenzi na usimamizi wa miradi na mifumo ya TEHAMA Serikalini.
Nitumie nafasi hii kutoa wito kwa Wizara, Wakala, Idara za Serikali, Taasisi na Mashirika ya Umma, Sekta Binafsi na wadau wote wa Serikali Mtandao kushirikiana kikamilifu na Mamlaka, katika kufanikisha malengo yetu ya kuleta mapinduzi ya kidijiti Serikalini na kufanya huduma za Serikali kuwa bora zaidi kwa mwaka mpya wa 2025.
Tunapenda kuwashukuru kwa ushirikiano wenu wa karibu mwaka uliopita na tunatarajia kuendelea kushirikiana kwa karibu zaidi kwa mwaka 2025.
Aidha, napenda kuchukua fursa hii kuwakaribisha wote katika Mkutano wa Tano (5) wa Mwaka wa Serikali Mtandao, utakaofanyika tarehe 11 – 13 Februari 2025, katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Arusha (AICC) jijini Arusha.
Katika kikao hiki, tutakuwa na fursa ya kujadili kwa pamoja na kuweka mikakati ya kuimarisha na kukuza jitihada za Serikali Mtandao katika Taasisi za Umma, na kuimarisha ushirikiano wetu ili kuhakikisha utoaji wa huduma serikalini kidijitali unaimarika zaidi.
Heri ya Mwaka Mpya 2025! Tushirikiane kwa pamoja katika safari hii ya kuijenga Serikali Kidijiti.