emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

RAIS DKT.SAMIA AWATAKA VIONGOZI WA UMMA KUTUMIA MFUMO WA e-MREJESHO KUPOKEA MAONI YA WANANCHI.


RAIS DKT.SAMIA AWATAKA VIONGOZI WA UMMA KUTUMIA MFUMO WA  e-MREJESHO KUPOKEA MAONI YA WANANCHI.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt Samia Suluhu Hassan, amewataka viongozi wa umma kutumia Mfumo wa Kielektroniki wa Mawasiliano wa e-Mrejesho ili kupokea maoni ya wananchi kuhusu Serikali na pia kutoa mrejesho kwa wananchi kupitia mfumo huo.

Dkt. Samia ametoa maelekezo hayo Machi 13 mwaka huu Ikulu jijini Dar es Salaam, mara baada ya kuwaapisha viongozi aliowateua katika nafasi mbalimbali wakiwemo Wakuu wa Mikoa, Katibu Mkuu, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri.

Alisema kuwa, viongozi wa umma wanapaswa kufahamu na kutumia mifumo mbalimbali ya TEHAMA iliyopo Serikalini katika utekelezaji wa majukumu yao, ikiwa ni pamoja na kutumia Mfumo wa e-Mrejesho kupokea maoni ya wananchi na kutoa mrejesho kwa wananchi pamoja na Serikali juu ya utekelezaji wa maoni hayo.

‘’Nendeni mkatumie mfumo wa e-Mrejesho nyie mpate mrejesho na sisi tupokee mrejesho lakini na wananchi wapate taarifa kupitia huu mfumo na ndivyo tutakavyoweza kufanya kazi kwa haraka na kwa ufanisi zaidi tukitumia mifumo’’, alisisitiza Rais Samia.

Alibainisha kuwa, viongozi wa umma wanapaswa kuitumia vizuri mifumo mbalimbali ya kielektroniki inayopelekwa Serikalini, ili isaidie kuongeza ufanisi wa utendaji kazi wao na kuimarisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi kwa wakati mahali walipo.

Akizungumza kuhusu matumizi ya mifumo ya TEHAMA Serikalini, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Mha. Benedict Ndomba amesema kuwa, e-GA itaendelea kusimamia matumizi ya TEHAMA Serikalini ili kuhakikisha yanaleta tija kwa kuongeza ufanisi wa utendaji kazi na kurahisisha upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi kwa wakati mahali walipo.

Alisema kuwa, moja ya eneo ambalo Mhe. Rais amekuwa akilipa kipaumbele ni kuimarisha Serikali Mtandao kwa kuhakikisha Taasisi za Umma zinatumia TEHAMA kwenye utendaji kazi wake na wananchi wanapata huduma za Serikali kidijatali mahali popote na muda wote.

“Katika kuhakikisha tunafikia lengo la Mhe. Rais, e-GA kwa kushirikiana na taasisi nyingine za umma tumetengeneza mifumo mbalimbali ya TEHAMA ambayo imesaidia kupunguza gharama, kuokoa muda, kuongeza ufanisi na kuwarahisishia wananchi kupata huduma za Serikalia kidijitali mahali walipo”, alifafanua Ndomba.

Aliongeza kuwa, mfumo wa e-Mrejesho unawawezesha wananchi kutuma kero au malalamiko, maoni, maswali, na pongezi kidijitali kwenda katika taasisi yoyote ya umma na kisha kupata mrejesho wa utekelezaji wake kidijitali mahali walipo.

Vilevile, Mfumo huu unasaidia kuokoa muda na fedha kwani mwananchi halazimiki tena kusafiri umbali mrefu kwenda katika ofisi ya umma kwa ajili ya kuwasilisha malalamiko yake au kufuatilia utekelezaji wake na badala yake anaweza kufanya hivyo kidijitali kupitia simu yake ya kiganjani mahali alipo, alisema Ndomba.

“Zamani ilikuwa mtu akihitaji kutoa maoni au malalamiko kuhusu huduma inayotolewa na taasisi ya umma ilimlazimu kufika katika taasisi hiyo na kuwasilisha malalamiko yake kwenye sanduku la maoni au kuwasilisha barua katika taasisi hiyo na kisha kufanya ufuatiliaji wa utekelezaji wake, lakini kwa sasa anaweza kuwasilisha maoni hayo kidijitali”, alifafanua Ndomba.

Alieleza kuwa, mfumo wa e-Mrejesho unapatikana kwa njia tatu ambazo ni kupitia simu ya mkononi kwa kubofya *152*00# na kisha kuchagua namba 9 na kisha namba 2, njia zingine ni kupitia simu janja kwa kupakua Aplikesheni (Mobile App) ya e-Mrejesho inayopatikana kwenye Play Store na Apple Apps Store, na kwa njia ya Tovuti ya emrejesho.gov.go.tz.

Aliongeza kuwa, ikiwa mwananchi atakosea kuwasilisha lalamiko lake katika taasisi husika, mfumo wa e-Mrejesho unaruhusu lalamiko hilo kuhamishwa kutoka taasisi moja kwenda taasisi nyingine na pia unamruhusu mwananchi kukata rufaa kwenda ngazi ya juu ya taasisi ikiwa hatoridhika na majibu yaliyotolewa kuhusu lalamiko lake.

Mfumo huu unasaidia kuongeza uwajibikaji, kwani lalamiko linapofika kwenye taasisi litaonekana kwenye ngazi zote za uongozi wa taasisi hiyo na kila Afisa aliyelifungua ama kulifanyia kazi ataonekana, pia mfumo unafanya uchambuzi wa taarifa na kumuwezesha Katibu Mkuu Ofisi ya Rais UTUMISHI na Katibu Mkuu Kiongozi kuona malalamiko yaliyowazi, yanayoshugulikiwa na yaliyokamilika kupitia Dashboard maalum”, alisema Ndomba.

Katika kuhakikisha mifumo ya TEHAMA Serikalini inawasiliana na kubadilisha taarifa Ndomba alibainisha kuwa, mfumo wa e-Mrejesho unao uwezo wa kubadilishana taarifa na mifumo mingine kupitia Mfumo wa Ubadilishanaji Taarifa Serikalini ‘Government Enterprise Service Bus-GovESB’ na tayari mifumo mbalimbali imeunganishwa na e-Mrejesho kupitia Mfumo wa GovESB.

Mfumo wa e-Mrejesho umetengezwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Taasisi zote za Umma zimeunganishwa.