emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

MFUMO WA GISP WASAIDIA KUONGEZA UFANISI WA MIRADI YA TEHAMA SERIKALINI


MFUMO WA GISP WASAIDIA KUONGEZA UFANISI WA MIRADI YA TEHAMA SERIKALINI


Uwasilishaji wa miradi ya TEHAMA Serikalini katika Tovuti ya Huduma za TEHAMA Serikalini (GISP), umetajwa kuongeza ufanisi wa miradi hiyo kutokana na kutolewa ushauri wa kitaalamu katika hatua za awali unaofanywa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), kabla ya utekelezaji wa miradi hiyo.

Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na Meneja wa Usimamizi wa Miradi ya TEHAMA kutoka Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Bw.Godfrey Masanja, wakati alipofanya mahojiano malum kwa njia ya simu na mwandishi wetu kuhusu umuhimu wa mfumo wa GISP katika kuongeza tija na ufanisi wa miradi ya TEHAMA Serikalini.

“Kwa mujibu wa kifungu Na. 24 cha Sheria ya Serikali Mtandao Na. 10 ya Mwaka 2019, Taasisi za Umma zinazokusudia kutekeleza miradi ya TEHAMA zinapaswa kuwasilisha taarifa za miradi hiyo kwa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA)kupitia Mfumo wa GISP, ili kupata kibali kabla ya kuanza kutekeleza miradi hiyo”, alisema Bw. Masanja.

Alifafanua kuwa, mfumo wa GISP una lengo la kuharakisha na kupunguza muda uliohitajika kuwasilisha maombi ya huduma kwa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), ukilinganisha na njia nyingine kama vile barua.

Alibainisha kuwa, mfumo huo umesaidia kuongeza ufanisi katika utendaji kazi wa Serikali kwani unarahisisha ufuatiliaji na upatikanaji wa mrejesho wa hatua za utekelezaji wa maombi ya huduma za TEHAMA yaliyowasilishwa na Taasisi za Umma kwa Mamlaka ya Serikali Mtandao

“Mfumo wa GISP umesaidia kurahisisha mchakato wa utoaji wa huduma za TEHAMA kwa kupunguza wingi wa taarifa, hatua na muda unaohitajika kuwasilisha na kupata huduma za TEHAMA” alisema Bw. Masanja

Aidha, Bw. Masanja alifafanua kuwa taarifa zinazowasilishwa kupitia mfumo wa GISP ni pamoja na andiko la mradi (Project Concept Note/Proposal) lililoidhinishwa na Kamati ya Usimamizi wa TEHAMA ya Taasisi (Institutional ICT Steering Committee), ambapo Mamlaka hufanya mapitio ya andiko la mradi huo lililoidhinishwa na kutoa kibali cha mradi huo ndani ya siku 14 tangu kuwasilishwa kwa taarifa za mradi.

Aliongeza kuwa, uwasilishwaji wa taarifa za miradi kwenye mfumo wa GISP umesaidia kupunguza urudufu wa jitihada kwa kuepuka ujenzi wa mifumo inayofanya kazi zinazofanana na hivyo kupunguza matumizi ya fedha yasiyo ya lazima katika utekelezaji wa miradi.

“e-GA inapokea na kupitia taarifa zote za miradi zinazowasilishwa na Taasisi za Umma, na kisha kutoa idhini au maelekezo mbadala ili kuondoa uwezekano na urudufu wa jitihada na kuepuka matumizi ya fedha yasiyo ya lazima”, alisisitiza Bw. Masanja.

Sambamba na hilo Bw. Masanja aliongezea kuwa, mfumo wa GISP umesaidia kuimarisha usalama wa mifumo ya TEHAMA Serikalini kwa kuzingatia matumizi ya teknolojia zinazoendana na mazingira ya sasa, na kuhakikisha mifumo inayopatikana baada ya utekelezaji wa miradi husika inakuwa na uwezo wa kubadilishana taarifa na mifumo mingine ya TEHAMA Serikalini.

Pia, Mfumo wa GISP umeiwezesha na kuipatia nafasi e-GA ya kutambua miradi ya TEHAMA inayokusudiwa au inayotekelezwa na Serikali, na kuweza kutoa ushauri wa kitaalam kwa wakati kwa watekelezaji wa miradi hiyo, alifafanua Bw. Masanja.

Naye Meneja wa Huduma za Sheria e-GA ASP Raphael Rutaihiwa alisema kuwa, kwa mujibu wa Sheria ya Serikali Mtandao Kifungu Na. 57 kinaielekeza e-GA kuchukua hatua stahiki kwa taasisi ambayo itakiuka taratibu za kuwasilisha taarifa za miradi ya TEHAMA kwenye mfumo, kwani kunainyima nafasi Mamlaka kushauri kwa wakati kuhusu utekelezaji wa miradi hiyo.

Bw. Rutaihiwa amezitaka Taasisi za Umma kuzingatia Sheria ya Serikali Mtandao kwa kuwasilisha taarifa za miradi ya TEHAMA kupitia GISP, kwa miradi yote inayotekelezwa na iliyokwisha kutekelezwa, pamoja na miradi yote ya TEHAMA inayokusudiwa kutekelezwa.

Akizungumzia taratibu za uwasilishwaji wa miradi kwenye mfumo huo, Bw. Masanja alisema Taasisi za Umma zinatakiwa kuandika barua kwenda Mamlaka ya Serikali Mtandao, kuomba kusajiliwa katika mfumo wa GISP ikiwa na taarifa za taasisi na wataalam wa TEHAMA wa taasisi hiyo wanaokusudiwa kufunguliwa akaunti katika mfumo wa GISP (majina, barua pepe na namba ya simu).

Aidha, Taasisi zilizowasilisha taarifa za miradi kwenye GISP na kupewa kibali cha kuendelea na utekelezaji wa miradi hiyo, zinatkiwa kuwasilisha taarifa za utekelezaji wa miradi hiyo kupitia GISP ili kuwa na taarifa sahihi za utekelezaji wa mradi, pamoja na kusaidia utoaji wa ushauri wa kitaalam kulingana na hali halisi ya utekelezaji wa miradi hiyo kwa vipindi husika, alisema Bw. Masanja.

Taasisi zinaweza kuwasiliana na dawati la msaada wa kiufundi la Mamlaka ya Serikali Mtandao kupitia barua pepe: egov.helpdesk@ega.go.tz au simu: 0764292299 au 0763292299 kwa msaada zaidi. Aidha, mfumo wa GISP unapatikana kupitia https://gisp.gov.go.tz.