Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora

Wakala ya Serikali Mtandao.

DUWASA kutumia huduma za Wakala

DUWASA kutumia huduma za Wakala

2015-07-06

Mamlaka ya Maji Safi na Mazingira DODOMA (DUWASA) imesema ipo tayari kutengenezewa tovuti, kusajiliwa na kutumia kikoa cha .go.tz, kutumia Mfumo wa Barua Pepe Serikalini, Masafa ya Serikali na kutengenezewa Mifumo itakayorahisisha utoaji huduma kwa Umma.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Mhandisi David Pallangyo kwenye kikao cha pamoja kati ya Wakala ya Serikali Mtandao na Menejimenti ya Mamlaka hiyo kilichofanyika mjini Dodoma.

“Tupo tayari kushirikiana na Wakala katika kazi zetu, pia tumeona ni muhimi kupata ushauri wenu wa kiufundi katika suala la TEHAMA ili kuweza kurekebisha mifumo tuliyonayo na kutoa huduma bora kwa wananchi”, alisema Pallangyo.

Wajumbe wa Menejimenti hiyo walitaka kufahamu kama Wakala inaweza kupata taarifa kutoka kwa mtoa huduma ya mtandao (Internet Service Provider) pindi tatizo la kimtandao linapotokea, ambapo Mkurugenzi wa Usimamizi wa Huduma za TEHAMA wa Wakala Bw. Benedict Ndomba alisema ni ngumu kwa Wakala kupata taarifa hizo ndio maana taasisi za Serikali zinashauriwa kutumia Mfumo wa Barua Pepe Serikalini (GMS) ili kama tatizo likitokea inakuwa rahisi kufahamu chanzo cha taarifa hiyo.

Akiwasilisha mada inayohusu Usimamizi wa yaliyomo katika tovuti, Meneja wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano cha Wakala Bi. Suzan Mshakangoto alisema ni muhimu Afisa Habari na Afisa TEHAMA kushirikiana katika kuhakikisha tovuti inapatikana na inakuwa na habari mpya.

“Ni jambo zuri kwa watumishi wa taasisi kuweza kusoma taarifa zilizo kwenye tovuti yao ili kama kuna upungufu na changamoto zilizojitokeza ziweze kushughulikiwa na tovuti hiyo kuwa na taarifa zilizokuwa hai”, alisema Mshakangoto.

Aidha Bi. Mshakangoto alisema Wakala inazingatia mwongozo wa kutengeneza tovuti za Serikali lakini pia inazingatia mabadiliko ya teknolojia katika kutengeneza tovuti hizo ikiwa ni pamoja na mwonekano wa tovuti husika.

Vilevile Mshakangoto aliishauri Mamlaka hiyo kuwa karibu na Wizara ya Habari, Elimu, Utamaduni na Michezo ili kama kuna maswali yoyote yaliyoulizwa na wananchi au kuna kero zilizoainishwa na wananchi zinazohusu DUWASA kupitia tovuti rasmi ya wananchi ziweze kutolewa majibu na Mamlaka hiyo.

 

Wakala ya Serikali Mtandao inatembelea taasisi za Serikali kwa lengo la kujitangaza na kunadi huduma mbalimbali zinazotolewa ili kuziwezesha taasisi hizo kutoa huduma bora kwa wananchi.