Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora

Wakala ya Serikali Mtandao.

“Mobile Platfoam” ni tija kwa ukusanyaji kodi-Sefue

“Mobile Platfoam” ni tija kwa ukusanyaji kodi-Sefue

2015-06-22

Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue amesema Mfumo wa Jukwaa la Vitumi vya Mkononi “Mobile Platform” utasaidia katika ukusanyaji wa kodi kwa Serikali za mitaa.

Balozi Sefue ameyasema hayo alipotembelea banda la Wakala ya Serikali Mtandao kwenye maonesho ya wiki ya Utumishi wa Umma katika viwanja vya mnazi mmoja juni 22, 2015.

Mtendaji Mkuu wa Wakala Dkt. Jabiri Bakari alimueleza Balozi Sefue kuwa Serikali Mtandao inatengeneza mifumo mbalimbali ikiwemo Huduma za Serikali kupitia simu za mkononi, Mfumo wa Huduma kwa Mteja na Mifumo mingine ili kuziwezesha taasisi za Umma kutoa huduma kwa wananchi kwa haraka na ufanisi.

Naye Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Prof. Mussa Assad alipotembelea banda la Wakala alifurahishwa na huduma zinazotolewa na kuona ni vema tovuti ya taasisi yake ihifadhiwe na Wakala pamoja na kutumia Huduma za Serikali kupitia simu za mkononi.

Wakati huohuo Balozi Ombeni Sefue amezindua rasmi mkataba wa Huduma kwa Mteja wa Bodi ya Mishahara na Maslahi katika utumishi wa Umma na amewataka watumishi wa Umma kuusoma na kuuelewa Mkataba huo ulioandaliwa na Bodi ya Mishahara na maslahi katika Utumishi wa Umma ili wafahamu yale yaliyoainishwa katika mkataba huo na kufuatilia ili kuhakikisha yote yanatekelezwa kama inavyokusudiwa.

“Lazima tuwe na utaratibu wa kuthamini kazi tunazozifanya ili kila mtu kwa kazi aliyonayo apate mshahara na maslahi katika hali nzuri”, alisema Sefue.

Kauli mbiu ya Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kwa mwaka 2015 ni ‘Utumishi wa Umma katika Bara la Afrika ni chachu ya kuwawezesha wanawake, kuongeza ubunifu na kuboresha utoaji huduma kwa Umma”.

 Maonesho hayo yaliyoanza Juni 16 yanatarajiwa kumalizika Juni 23, 2015 ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais mstaafu wa awamu ya pili, Mhe. Ally Hassan Mwinyi