Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora

Wakala ya Serikali Mtandao.

TFDA kutumia huduma za Wakala

TFDA kutumia huduma za Wakala

2015-06-12

Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) ipo tayari kutumia huduma ya Ujumbe Mfupi kupitia simu ya mkononi (GSMS), Mfumo wa Barua Pepe wa Serikali (GMS) na kutengenezewa Tovuti ili kurahisisha utoaji huduma kwa wananchi.

Hayo yamesemwa na Meneja wa TEHAMA wa Mamlaka hiyo Bw. Ambele Mwafula wakati wa kikao cha pamoja kati ya Wakala na Menejimenti ya taasisi hiyo kilichofanyika Juni 12, 2015 katika Ofisi za TFDA.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka  hiyo Bw. Hiiti .B. Siro amesema Wakala ya Serikali Mtandao ni moja ya taasisi inayofanya kazi nzuri na kwa kasi ya hali ya juu na ikienda na kasi hiyo itafikia malengo yake kwa muda mfupi.

 “Naipongeza Wakala kwa kutekeleza majukumu  yake ipasavyo kwa sababu ndani ya muda mfupi tangu kuanzishwa kwake tumeona mabadiliko makubwa katika taasisi za Umma hasa katika suala hili la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)”, alisema Bw. Siro.

Aidha Menejimenti hiyo ilitaka kufahamu lini matumizi ya karatasi Serikalini yatafika ukomo ambapo Mkurugenzi wa Uratibu wa Huduma za TEHAMA wa Wakala Bw. Benedict Ndomba alisema zipo juhudi zinafanyika za kupata Ofisi Mtandao (e- Office) na muda ukifika Serikali itahamia rasmi katika Mtandao huo.

Aidha, Meneja wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano cha Wakala, Bi. Suzan Mshakangoto alisema TFDA ni miongoni mwa taasisi ambayo imeweka taarifa zake vizuri katika Tovuti Kuu ya Serikali na hivyo walete matangazo yao ili wananchi wapate taarifa moja kwa moja kupitia tovuti hiyo.

Vilevile Bi. Mshakangoto alitumia fursa hiyo kuwakaribisha katika Mkutano wa mwaka wa Wakala utakaofanyika Jijini Arusha Agosti 17 hadi 19, 2015 jambo lililoungwa mkono na Menejimenti hiyo na kuthibitisha ushiriki wao katika Mkutano huo.

Wakala inafanya vikao na Menejimenti za taasisi mbalimbali za Umma ili kuweza kuitangaza Wakala na huduma zinazotolewa.