Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora

Wakala ya Serikali Mtandao.

Taasisi za Umma Zaridhia kutumia huduma za Wakala

Taasisi za Umma Zaridhia kutumia huduma za Wakala

2015-04-30

Taasisi tano (5) za Umma zimefurahishwa na huduma mbalimbali zinazotolewa na Wakala na zimeonesha utayari wa kuzitumia wakati wa vikao vya Menejimenti ya Wakala kwa taasisi hizo zilizofanyika kwa wakati tofauti katika ofisi zao Aprili, 2015.

Meneja kutoka Kitengo cha Elimu, Habari na Mawasiliano, Bi. Suzan Mshakangoto amezitaja taaasisi hizo kuwa ni Mfuko wa Pensheni ya Mashirika ya Umma (PPF), Ofisi ya Mhasibu Mkuu wa Serikali (ACGEN), Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Wizara ya Nishati na Madini na Manispaa ya Ilala.

Aidha, Bi. Mshakangoto amezitaja huduma hizo kuwa ni Mfumo wa barua pepe Serikalini, huduma za Serikali kupitia simu za mkononi, huduma ya masafa,  huduma za Serikali ya ujumbe mfupi (SMS), huduma ya vituo vya kurejesha data, mfumo wa kufuatilia mafaili  na mfumo wa ulipaji wa kielektroni.

 

“Huo ni mwitikio chanya kwa Wakala unaotupa faraja katika kuendelea kutoa huduma zetu kwa taasisi za Umma”, alisema Bi. Mshakangoto.

Ameongeza kuwa, taasisi nyingine zinazotarajiwa kufanya kikao na Wakala ni, Wizara ya Kazi na Ajira, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Bohari Kuu ya Dawa (MSD).

Wakala iliomba vikao na Menejimenti za taasisi 40 za Umma ili kuzitangaza huduma mbalimbali zinazotolewa na Wakala katika utekelezaji wa Serikali Mtandao nchini.