Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora

Wakala ya Serikali Mtandao.

Mafunzo ya Ukaguzi wa ndani yatolewe kwa wingi

Mafunzo ya Ukaguzi wa ndani yatolewe kwa wingi

2015-05-27

Mtendaji Mkuu wa Wakala Dkt. Jabiri Bakari amemtaka Mkuu wa Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani kuandaa mafunzo mbalimbali ya ukaguzi wa ndani yatakayoshirikisha watumishi wengi zaidi ili kuweza kuongeza wigo wa uelewa na ujuzi wa fani hiyo.

Dkt. Bakari ameyasema hayo kwenye mafunzo ya kamati ya ukaguzi wa ndani iliyofanyika katika ofisi za Wakala Mei 27, 2015.

“Wakala imejitengenezea utaratibu wa kufanya kazi kwa kuzingatia namna biashara zinavyoendeshwa na hivyo tunataka ukaguzi wa ndani uisaidie taasisi katika utendaji kazi wake wa kila siku ili iwe moja kati ya taasisi za Serikali zinazofanya vizuri”, alisisitiza Dkt. Bakari.

Mwezeshaji wa mafunzo hayo kutoka Joint Finance Community Bw. Cassim Mambo, amesema wakaguzi wa ndani wanatakiwa kufuata taratibu, sheria na kanuni zilizowekwa katika utendaji kazi ili kuongeza ufanisi na tija kwa Serikali.

Naye Mkaguzi Mkuu wa Ndani kutoka Internal Auditor General Bw. Alphonce Muro amesema ifike mahali kamati ya ukaguzi wa ndani ya eGA iwe ni mfano wa kuigwa ili wakala nyingine zijifunze kupitia kwao.

Mkurugenzi wa Huduma na Biashara Bw. Ibrahim Mahumi amesema ni muhimu kwa watumishi wa Wakala kushirikiana na wakaguzi wa ndani katika kutekeleza majukumu yao ili kuweza kufikia malengo kwa kuwa wakaguzi hao wapo kwa ajili ya kujenga.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Bw. Eric Kitale amesema ujuzi na maarifa yaliyopatikana katika mafunzo hayo yatasaidia katika kuboresha utendaji kazi wa taasisi.

Kamati hiyo yenye wajumbe watano, watatu kutoka Wakala ya Serikali Mtandao na wengine wawili kutoka taasisi nyingine za Serikali inatarajiwa kufanya kazi zake kwa uadilifu na kwa uhuru ili kuiwezesha Wakala kufikia malengo yaliyowekwa.