Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora

Wakala ya Serikali Mtandao.

Maofisa TEHAMA waaswa kuzingatia Mafunzo ya uendeshaji wa vituo vya data

Maofisa TEHAMA waaswa kuzingatia Mafunzo ya uendeshaji wa vituo vya data

2015-03-17

Maofisa TEHAMA kutoka taasisi mbalimbali za Serikali wametakiwa kuzingatia na kushiriki kwa ukamilifu katika mafunzo yanayohusu uendeshaji wa vituo vya data (data centres) ili kuweza kuendesha vituo hivyo kikamilifu.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Udhibiti wa Huduma za TEHAMA wa Wakala ya Serikali Mtandao, Bw. Michael Moshiro alipofungua mafunzo ya siku tatu (3) ya Uendeshaji wa vituo vya data yaliyoandaliwa na kampuni ya “dimention data” kwa kushirikiana na Wakala yaliyofanyika Bahari Beach, Machi 17-19, 2015.

“Ushirikiano kati ya Wakala na taasisi binafsi ni muhimu katika kufanikisha utoaji na upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi kwa wakati muafaka”. Alisema Bw. Moshiro.

Naye Mkurugenzi wa Miundombinu na Uendeshaji (DCIO) Bw. Benjamin Dotto amesema taasisi binafsi zinasaidia katika kuongeza ubunifu na kutoa majibu ya masuala mbalimbali ambayo hutumiwa na Serikali katika kutoa huduma kwa wananchi.

“Ni matarajio ya Wakala kuwa baada ya mafunzo haya, washiriki watatumia ujuzi waliopata katika kuzishauri taasisi zao na Serikali kwa jumla katika suala la matumizi bora ya vituo vya data”. Alieleza Bw. Dotto.

Aidha, Meneja wa Idara ya Mtandao wa Serikali (GovNet) Bw. Ricco Boma alisema, mafunzo hayo yanahusu masuala ya teknolojia kwa vituo vya data, namna vituo hivyo vinavyofanya kazi na jinsi ya kuvitunza.

Mafunzo hayo ya siku tatu yalihudhuriwa na taasisi za Umma ikiwemo Wakala ya Serikali Mtandao (eGA), Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TASUBA) na Wakala ya Huduma za Ununuzi Serikalini (GPSA).