Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora

Wakala ya Serikali Mtandao.

Miaka mitano ya eGA yafungua njia ya TEHAMA

Miaka mitano ya eGA yafungua njia ya TEHAMA

2017-12-21

Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali Mtandao, Dkt. Jabiri Bakari amesema Wakala imefanikiwa Kusimamia utekelezaji wa Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao kwa taasisi za umma ili kuwezesha utekelezaji wa serikali mtandao, pia inatumia viwango na miongozo hiyo kutoa maelekezo ya namna sahihi ya kutekeleza jitihada za serikali mtandao na kupunguza urudufu.

Dtk. Bakari amesema hayo leo wakati wa kikao cha pamoja na wahariri wa vyomba vya habari ambapo alizungumzia mafanikio lukuki yaliyopatikana ndani ya miaka mitano ya wakala kuanzia mwaka 2012/13 hadi 2016/17 katika utekelezaji wa serikali mtandao nchini.

Vilevile amesema, Wakala imeendesha vituo vya Kuhifadhi Mifumo na Data za Serikali vinavyotoa huduma za kuhifadhi tovuti, mifumo tumizi, utunzaji katika sehemu zaidi ya moja, “co-location” na usajili na uhifadhi wa majina miliki. 

“Kwa miaka hii mitano, tumeweza kutengeneza na kuendesha Mtandao wa Mawasiliano Serikalini (GovNet) ulio salama na nafuu ambapo taasisi za umma 150 zikiwemo Wizara na Idara za Serikali, Hospitali za Mikoa na baadhi ya Ofisi za halmashauri zimeunganishwa ndani ya mtandao huu”, alifafanua Dkt. Bakari.

Ameongeza kuwa, katika utoaji wa utoaji wa huduma za ushauri wa kitaalamu, taasisi za umma 299 zimepatiwa ushauri na huduma za msaada wa kiufundi 2947 katika maeneo ya Uhakiki wa Mifumo ya TEHAMA, Tathmini ya Usalama wa TEHAMA, Utengenezaji wa Mpango wa Kukabili Majanga, Utayarishaji wa Mkakati wa TEHAMA, Utayarishaji wa Sera ya TEHAMA, na Utayarishaji na Usanifishaji wa Shughuli na Uhakiki wa Miradi ya TEHAMA. 

Aidha amesema, Wakala hiyo imafanikiwa kutoa mafunzo ya kiufundi ya serikali mtandao katika maeneo ya usimamizi wa mtandao  kwa taasisi 240, Mfumo wa Baruapepe Serikalini kwa taasisi 359, utekelezaji wa huduma mtandao kwa taasisi 76 na usimamizi wa tovuti kwa taasisi 411.  

“Tumehuisha na kusanifu upya Tovuti ya Serikali kuwa Tovuti Kuu (www.tanzania.go.tz ) ambayo ni kituo kimoja cha kutolea taarifa na huduma mtandao kwa wananchi kwa kupitia sehemu ya huduma za simu za mkononi na wavuti ya tovuti hii na hivyo, wananchi wananufaika kwa kupata taarifa mbalimbali za Serikali kwa urahisi”, alisema Dkt. Bakari.

Vilevile amesema, Wakala imetengeneza na kuendesha Mfumo wa Huduma za Serikali kwa kutumia Simu za Mkononi (mGOV) kama kituo kimoja cha huduma zote za Serikali kwa simu za mkononi, ambapo jumla ya taasisi za umma 117 zinatumia mfumo huo na zaidi ya miamala 15 milioni imefanywa.

Aidha, Wakala imesanifu na kutengeneza Mfumo wa Ofisi Mtandao (GeOS) ambao unatumika kuwezesha shughuli za kila siku za utawala za ofisi Serikalini ndani na miongoni mwa taasisi za umma ambapo hadi sasa taasisi za umma 28 zimeunganishwa na kutumia mfumo huo. 

“Tumesanifu na kutengeneza Mfumo wa Serikali wa Baruapepe (GMS) unaowezesha mawasiliano ya ofisi ambapo jumla ya taasisi za umma 359 zikiwemo   ofisi za Ubalozi zimeunganishwa na zinatumia mfumo huu”, alifafanua Dkt. Bakari.

Aidha amesema, Wakala imewezesha usanifu na utengenezaji wa mifumo mbalimbali inayowesesha utendaji kazi katika Taasisi za Umma ikiwemo Mfumo wa wa kutoa taarifa za ruswa (TAKUKURU kupitia namba 113), Mfumo wa Taarifa na shughuli za Bunge, Mfumo wa Ajira unaorahisisha mchakato wa ajira za Serikali na Mfumo wa Malipo ya Serikali kielektroni(GePG) unaowezesha udhibiti wa ukusanyaji wa Maduhuli kielektroni Serikalini.

Wakala ya Serikali Mtandao ilianzishwa 2012 kwa Sheria ya Wakala za Serikali Na.30 ya Mwaka 1997 Sura ya 245 na Kanuni zake. Wakala hii ina jukumu na mamlaka ya kuratibu na kusimamia utekelezaji wa Serikali Mtandao kwa Taasisi za umma. Lengo ni kuziwezesha Taasisi hizo kutumia TEHAMA katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuongeza ufanisi, uwajibikaji na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.