Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora

Wakala ya Serikali Mtandao.

Maabara, Sukari na Msajili wapatiwa mafunzo

Maabara, Sukari na Msajili wapatiwa mafunzo

2017-06-19

 Watumishi 11 kutoka Maabara ya Taifa ya Uvuvi (NFQCLAB), Bodi ya Sukari Tanzania (SBT) na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa (ORPP) wamepata mafunzo ya kukusanya, kupandisha na kuhuisha taarifa kwenye tovuti zao zilizotengenezwa na kusanifiwa na Wakala ya Serikali Mtandao (eGA).

 Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Ofisa TEHAMA kutoka Maabara ya Taifa ya Uvuvi,  Bw.Kirama Khalid amesema taasisi yao haikuwa na tovuti, jambo lililochangia wananchi kutofahamu kazi mbalimbali wanazozifanya.

 “Tumekuwa tukifanya mambo mengi sana kama taasisi lakini wananchi hawafahamu, hivyo naamini sasa kwa uwepo wa tovuti ya NFQCLAB, itakayopatikana kupitia www.nfqclab.go.tz kutaifanya jamii  kuelewa kwa upana juu ya taasisi hii ikiwemo huduma tunazozitoa pamoja na miradi mbalimbali inayoendelea katika maabara hii”, amesema Bw. Khalid.

 Naye Ofisa TEHAMA Mwandamizi kutoka Bodi ya Sukari Tanzania, Bw. Geofrey Matipani amesema kuwa Bodi ya Sukari Tanzania (SBT) itatumia fursa hii ya tovuti, kupitia www.sbt.go.tz kutoa elimu kuhusu shughuli zinazofanywa na kutekelezwa kwa mujibu wa sheria na hivyo wananchi kupata taarifa sahihi na kwa wakati.

Bi. Jacqueline Kilama kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa  amesema tovuti yao mpya, itakayopatikana kupitia anuani www.orpp.go.tz itakuwa na taarifa zote muhimu zinazohusiana na masuala mbalimbali ya vyama vya siasa, ikiwa ni pamoja na orodha kamili ya vyama vya siasa nchini vilivyosajiliwa, taratibu za kusajili chama cha siasa, kufuta chama cha siasa pamoja na huduma mbalimbali zinazotolewa na Ofisi hiyo.

 “Naipongeza sana eGA  kwani sasa wananchi wananufaika kwa kupata taarifa za Serikali na huduma zinazotolewa na taasisi husika kupitia tovuti zao. Naamini wananchi watanufaika na uwapo wa tovuti yetu”, alisema Bi. Jacqueline.

 Wakala imekuwa ikisanifu na kutengeneza tovuti mbalimbali za Serikali ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa kwa umma. Pia imekuwa ikiendesha mafunzo ili kuwajengea uwezo na ujuzi maafisa mbalimbali wa kuandaa, kuhuisha na kupandisha taarifa mbalimbali za taasisi kwa ajili ya tovuti zao. Mafunzo hayo yamefanyika katika ofisi za Wakala kwa muda wa siku tano kuanzia Juni 12 hadi 16, 2017.