Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora

Wakala ya Serikali Mtandao.

Viwango na Miongozo ya TEHAMA Serikalini Kurahisisha Utoaji Huduma kwa wananchi

Viwango na Miongozo ya TEHAMA Serikalini Kurahisisha Utoaji Huduma kwa wananchi

2016-11-10

Serikali imeandaa Muundo wa Viwango na Miongozo wa Serikali Mtandao unaotosheleza mahitaji ya usanifishaji wa shughuli za serikali Mtandao ambao unahakikisha serikali inakuwa kama taasisi moja kwa kuunganishwa na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) huku usalama na faragha za taarifa za serikali na watumiaji zikiimarishwa.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Udhibiti wa Huduma za Serikali Mtandao, Bw. Michael Moshiro katika mafunzo maalum ya kuwaelimisha  waandishi wa habari umuhimu wa kuzingatia viwango na miongozo ya usanifishaji shughuli za serikali mtandao kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Wakala ya Serikali Mtandao(eGA) Novemba 10,2016.

Bw. Moshiro amesema, lengo kuu la muundo wa viwango na miongozo hiyo ni  kurahisisha utendaji kazi wa serikali na kuboresha kwa kiasi kikubwa  utoaji wa huduma kwa wananchi.

“Miongozo hiyo inahusu maeneo  mbalimbali ambayo ni Usanifishaji Programu Tumizi za Serikali, Usanifishaji wa Shughuli za Serikali Mtandao, Usanifishaji wa Taarifa za Serikali Mtandao, Usanifishaji wa Miundombinu ya Serikali Mtandao na  Mfumo wa Serikali Mtandao Kuwasiliana. Maeneo mengine ni  Usanifishaji wa Usalama wa Serikali Mtandao, Usanifishaji wa Dira ya Serikali Mtandao, Usanifishaji Utangamanishi wa Serikali Mtandao pamoja na Mchakato wa Serikali Mtandao na Usimamizi”, alifafanua Bw. Moshiro.

Vilevile amesema, Serikali pia imeandaa miongozo mbalimbali inayosimamia utekelezaji wa baadhi za operesheni za TEHAMA kwenye eneo la Mawasiliano kwa Njia ya Video Serikalini, Tovuti na Mifumo Serikalini, Mwongozo katika Mifumo ya Sekta ya Afya, Uingizaji Taarifa kwenye Mifumo ya TEHAMA, Miradi ya TEHAMA na Huduma za Serikali kwa Njia ya Simu.

Ameongeza kuwa, mbali na hayo Serikali imefanya jitihada mbalimbali kuhakikisha Sera, Sheria, Miongozo na Mikakati madhubuti inayotumika katika utekelezaji wa Jitihada za Serikali Mtandao  inatumika katika hatua mbalimbali kuanzia ngazi ya Taifa hadi ngazi ya Taasisi husika.

“Kwa upande wa Sera, kuna Sera ya Taifa ya TEHAMA na Mpango Mkakati wa Serikali Mtandao, zipo sheria zinazosimamia Sekta ya TEHAMA nchini kama vile sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta ya mwaka 2010, Sheria ya Makosa ya Kimtandao pamoja na Sheria ya Miamala ya Kielektroni ya mwaka 2014”, alisema Bw. Moshiro.

Vilevile amesema, upo Waraka wa Utumishi Na. 5 wa Mwaka 2009 na Waraka Na. 3 wa Mkuu wa Utumishi wa Umma wa Mwaka 2003 unaohusu matumizi ya TEHAMA Serikalini pamoja na Mwongozo wa Matumizi Bora, Sahihi na Salama ya Vifaa vya TEHAMA Serikalini.

Ameeleza kuwa, pamoja na maendeleo na faida ambazo Serikali imezipata katika matumizi ya TEHAMA kwa kipindi kirefu, bado kulionekana kuwapo kwa changamoto nyingi ambazo zilikwamisha au kuchelewesha kufikiwa kwa malengo yaliyokusudiwa.

Amezitaja changamoto hizo kuwa ni, Utengenezaji au Ununuzi wa Mifumo ya TEHAMA isiyozingatia Mahitaji halisi ya taasisi na Serikali kwa jumla na uwapo wa mifumo inayoweza kuhatarisha usalama wa taarifa za Serikali.

“Changamoto hizo na nyingine kadha wa kadha ndizo zilizosababisha Serikali kuweka miongozo na viwango thabiti katika TEHAMA itakayowezesha Taasisi za Serikali kuzikabili”, alieleza Bw. Moshiro.

Akizungumzia faida za kuwa na Viwango na Miongozo, amesema itawezesha mifumo kujengwa kwa kuzingatia mahitaji halisi ya taasisi husika na Serikali kwa jumla, itasaidia uwapo wa mifumo na miundombinu ambayo ni endelevu baada ya kujengwa, itaondoa urudufu wa miundombinu na mifumo ya TEHAMA Serikalini pamoja na kuwezesha mifumo kuweza kubadilishana taarifa na hivyo kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Faida nyingine ni kupunguza gharama kubwa ya ujenzi na uhudumiaji wa mifumo ya TEHAMA, kuwezesha utumiaji wa rasilimali shirikishi na kupunguza gharama za utekelezaji wa jitihada mbalimbali za TEHAMA pamoja na Kuwezesha mifumo inayojengwa kuweza kutumiwa kiurahisi na walengwa wa huduma husika.

Aidha, amewashauri wadau wa sekta binafsi wanaojihusisha na utoaji wa huduma za TEHAMA na Ujenzi wa Mifumo ya TEHAMA kuwa na uelewa wa viwango na miongozo iliyopo ili waweze kuisaidia Serikali. Pia, amesema ni muhimu kwa wataalamu wa TEHAMA wanaotaka kufanya kazi na Serikali kuanza kujenga mifumo inayozingatia viwango vilivyopo kwa kuwa ni uamuzi wa Serikali kuanza kutumia miongozo na viwango hivyo.

“Viwango na Miongozo hii ipo kwenye tovuti ya Wakala inayopatikana kwa anwani ya www.ega.go.tz sehemu ya Viwango na Miongozo na inaendelea kuboreshwa kadiri ya mahitaji yanavyojitokeza”, alisisitiza Bw. Moshiro