emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

WAZIRI MHE. JENISTA MHAGAMA AZINDUA MFUMO WA HCMIS


WAZIRI  MHE. JENISTA MHAGAMA AZINDUA MFUMO WA HCMIS


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama,amezindua mfumo wa Kielektroni wa Tathmini ya Hali ya Watumishi katika Utumishi wa umma (HCMIS) unaolenga kubaini mahitaji halisi ya watumishi kwenye Wizara na Taasisi za Umma.

Wakati wa uzinduzi huo uliofanyika Machi 24,2022 jijini Dodoma Waziri Mhagama, amesema kuwa mfumo huo utawezesha ukusanyaji, uchakataji na uchambuzi wa taarifa za Watumishi kwa njia ya kisayansi ili kubaini mahitaji halisi ya Watumishi katika Wizara na Taasisi za Umma.

Waziri Mhagama amesema kuwa mfumo huo utasaidia kutathmini hali ya Watumishi waliopo na wanaohitajika katika taasisi zote za umma ili kuwapanga kwa kuzingatia mahitaji halisi ya kila taasisi.

“Kwa kutumia mfumo huu, Serikali itakuwa na taarifa na takwimu sahihi kuhusu watumishi waliopo, mahitaji ya watumishi wanaohitajika katika kutekeleza majukumu ya kuwahudumia wananchi,”amesema Mhagama.

Vilevile, Waziri Mhagama amewaagiza waajiri wote kuwasimamie Wakurugenzi au Wakuu wa Idara/Sehemu zinazosimamia Rasilimaliwatu katika taasisi zao kukamilisha zoezi la kuingiza taarifa za watumishi wao katika mfumo kabla ya tarehe 31 Machi, 2022.

“Ni imani yangu kuwa, wakuu wa taasisi za umma watazingatia maelekezo niliyotoa na yale ambayo yamekuwa yakitolewa kwa ajili ya kulifanya zoezi hili liwe na tija. “ameeleza.

Aidha, Mhe. Mhagama ameongeza kuwa taasisi ambazo hazitakamilisha zoezi hilo kwa muda uliowekwa zitakuwa zimekiuka maelekezo ya Serikali na hatua stahiki zitachuliwa dhidi yao.

“Kwa taarifa tulizonazo mpaka leo kati ya Wizara na Taasisi 427 zilizo kwenye Mfumo wa HCMIS, zote zimeshaanza kutumia Mfumo na zipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji wa zoezi hili na zipo kati ya asilimia 13 hadi 97. “amesema Mhagama

Waziri Mhagama amezitaja Taasisi 10 zilizofanya vizuri katika kuingiza taarifa za watumishi wao kwenye mfumo huo kuwa ni pamoja na Shule ya Sheria Tanzania (97%), Tume ya Ushindani (97%), Chuo cha Ardhi Morogoro (97%), Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala (96%) na Ofisi ya Rais Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa (95%).

Ofisi nyingine ni Sekretarieti ya Mkoa wa Iringa (95%), Wakala ya Mafunzo ya Mifugo (95%), Mamlaka ya Serikali Mtandao-eGA (95%),Taasisi ya Utafiti wa Wanyama Pori (95%) na Wakala ya Mafunzo ya Menejimenti ya Elimu (94%)