Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Abdallah Chaurembo ameipongeza Serikali kupitia Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) kwa kubuni mifumo inayotatua kero za wananchi wakati wa kutoa huduma kwenye taasisi za umma na kuwapa fursa ya kujibiwa kero zao hapo kwa papo.
Mhe. Chaurembo ameyasema hayo hivi karibu katika kikao kazi cha Kamati yake na Uongozi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kilichofanyika katika Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Maendeleo cha Mamlaka ya Serikali Mtandao Kilichopo Jijini Dodoma.
“Taasisi hii imefanya na inaendelea kufanya jitihada mbalimbali za kuwasogezea karibu huduma wananchi kwa ufanisi, haraka na gharama nafuu na kamati yangu itaendelea kuunga mkono jitihada hizo na wajumbe wawaelimishe wananchi kutumia mifumo ya TEHAMA katika maeneo yao ya utawala” amesisitiza Mhe. Chaurembo.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema kwa kutumia wataalamu wa ndani, Mamlaka ya Serikali Mtandao imekuwa ikibuni mifumo mbalimbali kwa lengo la kusogeza huduma za Serikali karibu na wananchi.
Mhe. Mchengerwa ametoa mfano wa Mfumo wa Sema na Waziri wa Utumishi (SWU) unaomwezesha mwananchi kuwasilisha kero na malalamiko moja kwa moja kwake na kufanyia kazi na kuwataka wajumbe wa kamati hiyo kutumia mfumo huo pia.
“Mkiwa wawakilishi wa wananchi tunawaomba mtusaidie kufikisha ujumbe kwa wananchi kuhusu mfumo huu ili kupunguza kabisa malalamiko na kutatua changamoto sugu za utumishi zinazowakabili watumishi wa umma. Aliongeza Mhe. Mchengerwa.
Mhe. Mchengerwa ameishukuru kamati kwa kuiongoza na kuishauri vema ofisi yake na kuahidi kuendelea kutekeleza maelekezo yote yanayotolewa na kamati hiyo kwa maslahi ya Taifa.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya eGA mbele ya kamati hiyo, Mhandisi Benedict Benny Ndomba, amesema Kituo hiki kinafanya kazi zake kwa kuzingatia falsafa ya kutumia wataalamu wa ndani kujenga mifumo ya TEHAMA kutatua matatizo yetu wenyewe na kuepuka utegemezi.
“Kupitia Kituo hiki, tunaelenga kwenye ubunifu na utafiti katika TEHAMA ili kuwa na mifumo itakayoboresha utoaji wa huduma kwa wananchi” ameongeza Injinia Ndomba.